Ulifahamu kuwa vitunguu vinatumika kufukuza wadudu shambani?
KANDO na kutumika kama kiungio kwenye mapishi, vitunguu vina manufaa tele kwa wakulima.
Aghalabu, maboma mengi hutumia vitunguu kwenye mapishi, kuunda saladi na kachumbari ili kuongeza ladha ya mlo.
Wakulima wanaofahamu tija zake, vitunguu ni dhahabu shambani.
Vipo vya mviringo (red bulb onions) na majani, japo vimegawanywa zaidi kwa mujibu wa familia na spishi.
Sam Nderitu, Afisa Mkuu Mtendaji Grow Biointensive Agriculture Center of Kenya (G-BIACK), ni kati ya wakulima wanaotumia vitunguu kukabiliana na kero ya wadudu.
G-BIACK ni kituo chenye makao makuu Thika, Kiambu ambacho kinajishughulisha na ufufuaji wa kilimo asilia.
Ukikizuru, lengo lake hasa likiwa ni utafiti wa kilimo asilia, kila kipande cha shamba hutakosa kuona vitunguu vikinawiri.
“Vitunguu ni miongoni mwa mimea ambayo haielewani na wadudu, huvitumia kuwafukuza (pest repellant),” Nderitu anadokeza.
Badala ya mkulima kuwa mtumwa wa dawa zenye kemikali kupulizia mimea na mazao yake shambani dhidi ya wadudu, anahimizwa kukumbatia mbinuhai kukabiliana nao.
Vinapaswa kupandwa kati ya mimea na vilevile kandokando mwa shamba.
“Ni nadra sana vitunguu kushambuliwa na wadudu, hivyo basi ni mimea bora kuwatimua,” anashauri mtaalamu Daniel Mwenda, mwaanzilishi Mwenda (D) Agroforestry Solutions.
Matumizi ya vitunguu kukabiliana na kero ya wadudu shambani, ni kati ya mbinu asilia ambazo wakulima wanaweza kukumbatia ili kuzalisha mazao salama.