Hadhi hafifu ya udongo inavyoweza kufufuliwa
HADHI ya udongo kufifia ni kati ya changamoto zinazozingira Sekta ya Kilimo Kenya.
Udongo umedhoofika kiasi kwamba kiwango cha uzalishaji chakula shambani kimepungua mara dufu.
Mababu zetu waliokuwa wanafanya kilimo miongo minne hivi iliyopita, ukipata fursa ya kutangamana na mmoja wao atakuelezea jinsi mashamba yalikuwa yakitoa mazao.
Yalikuwa yenye rutuba kwa sababu hayakuathirika na matumizi ya fatalaiza zenye kemikali.
Kwa sasa, mambo ni tofauti kabisa.
Mfano, ekari moja ya mahindi, wataalamu wanahoji inapaswa kuzalisha magunia yasiyopungua 40 ya kilo 90 kila moja.
Kwa sasa, wakulima wengi wanazalisha wastani wa magunia 10 katika kila ekari.
“Utafiti na ukaguzi unaonyesha udongo wa mashamba nchini umedhoofika sana,” anasema Dkt David Kamau, Mkurugenzi Kitengo cha Mazingira na Maliasili katika Shirika la Utafiti wa Uimarishaji Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro).
Afisa huyu anakadiria zaidi ya asilimia 60 ya ardhi ya Kenya imeathirika, hasa kutokana na matumizi ya pembejeo (fatalaiza na dawa) zenye kemikali.
Isitoshe, Dkt Kamau ananyooshea kidole cha lawama mafuriko, ufugaji mifugo kupita kiasi kwenye eneo dogo la shamba (over grazing) na ukame kuchangia hali kuwa mbaya zaidi.
“Maeneo kame (Asal), hasa, yameathirika pakubwa,” anasema mtafiti huyu.
Ni hali inayochochea taifa kushindwa kuzalisha chakula, Serikali ikisalia na chaguo la kukiagiza nje ya nchi.
Wizara ya Kilimo inakiri Serikali hutumia mabilioni ya pesa kununua chakula nje ili kuziba mwanya uliopo katika jitihada zake kukabiliana na njaa na usalama wa chakula nchini.
Hata ingawa ni zoezi linalochukua muda mrefu, Sam Nderitu, Afisa Mkuu Mtendaji Grow Biointensive Agriculture Center of Kenya (G-BIACK), anasema uwezekano upo kurejesha hadhi ya udongo.
G-BIACK ni kituo chenye makao makuu yake Thika, Kiambu ambacho kinajishughulisha na ufufuaji wa kilimo asilia.
Anasema, siri ni wakulima kurejelea kilimo asilia.
Kilimo asilia, mtafiti huyu anasisitiza ni matumizi ya mbolea isiyo na chembechembe zozote za kemikali.
“Matumizi ya mbolea ya mifugo, kwa mfano, ikichanganywa na majani na matawi ya mimea, yatasaidia kurejesha rutuba udongoni,” Nderitu anasema.
Hata hivyo, anasema ni mbolea ambayo mwanazaraa ana uhakika na chanzo chake.
“Kusiwe na chochote kinachotolewa nje ya boma la mkulima. Isitoshe, mifugo walishwe chakula na wapewe madini yasiyo na chembechembe zozote za kemikali. Kinyeshi chao kitakuwa mbolea asilia,” anafafanua.
Katika mukhtadha huohuo, Nderitu anasisitiza mimea ambayo majani na matawi yake yatatumika kupiga jeki mbolea ya ng’ombe, pia ikuzwe bila kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali.
“Itakuwa kazi bure kutumia mbolea yenye kemikali kujaribu kufufua hadhi ya udongo”.
Hiyo ni shughuli inayochukua muda, Nderitu akikiri pia ni ghali.