• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Je, Gor bado ina nafasi ya kuingia mechi za makundi CAF?

Je, Gor bado ina nafasi ya kuingia mechi za makundi CAF?

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia wanaamini mabingwa hawa wa Kenya wameshaaga soka ya Kombe la Mashirikisho la Afrika baada ya kuruhusu New Star ya Cameroon kupata bao la ugenini katika ushindi wao wa mabao 2-1 jijini Nairobi.

Wanasema matokeo haya katika mechi ya mkondo wa kwanza yaliwaudhi, ingawa sehemu ndogo ya mashabiki bado ina imani Gor haijapoteza kila kitu.

Haya hapa maoni yao:

Apong Kor, “Mabao haya ya ugenini kila mara hutuvuruga! Ni wazi Gor iko nje ya mashindano haya.”

Ephraim Obiero Akumu, “Masaibu yetu ya bao la ugenini…Tunahitaji kuongeza bidii na kuwa werevu katika mechi ijayo.”

Joji Poji, “Bao la ugenini??? Lazima pia mfunge bao nchini Cameroon. Sioni matumaini hapa.”

Otieno Onyango, “Tuliongoza 3-1 dhidi ya Lobi Stars (kabla ya mechi ya marudiano ya Klabu Bingwa Afrika)…hatujafanya chochote (nyumbani dhidi ya New Star).”

Tom Otieno, “Kwanini Gor hufungwa bao katika ardhi yake? Wanastahili kujizatiti kutofungwa nyumbani kwa sababu inatuweka katika hali ngumu tunapoenda kusakata mechi za marudiano!”

Robi Robert, “Ni kweli hamko salama, lakini leo (Jumapili) mliibuka na ushindi na mnastahili pongezi. Endeni Cameroon na mfunge bao.”

Sadia Jnr, “Hatukufaulu kusonga mbele tukiongoza (Lobi Stars) 3-1 katika Klabu Bingwa Afrika. Sijui mtanishawishi vipi kwamba tutafaulu kubandu nje New Star tunapoongoza 2-1?”

Fred Omondi, “Hilo bao la ugenini tena!”

Jay Pius Baraza, “Matatizo ya bao la ugenini.”

Prince Victor, “Bao hili la ugenini litanikosesha usingizi hadi mechi ya marudiano.”

Baadhi ya mashabiki waliendelea kumkosoa Kocha Mkuu Hassan Oktay akiwemo Peter Okech, ambaye alisema Mturuki huyo “si kocha.” Abuor Goerge Nicholas aliongeza, “Hata mechi za nyumbani inaonekana kuzishinda ni kupitia juhudi za wachezaji tu, natilia shaka uwezo wa kocha kuletea klabu hii matunda.”

Hofu ya mashabiki wa Gor kwamba timu yao huenda isipite awamu hii ya kutafuta tiketi ya kuingia mechi za makundi ina ukweli fulani wa kitakwimu unaoonesha miamba hawa wa Kenya wanapata ugumu sana kupata matokeo mengine ugenini isipokuwa kichapo.

Tangu mwaka 2009, mwaka ambao Gor ilirejea katika mashindano ya Afrika baada ya kuwa nje kwa muda mrefu, imeshinda mechi mbili pekee nje ya Kenya. Ilichapa Anse Reunion ya Ushelisheli 5-0 Machi 2, 2015 na Young Africans almaarufu Yanga kutoka Tanzania 3-2 Julai 29, 2018.

Imetoka sare mara mbili na kupoteza 12 zikiwemo tatu zilizopita dhidi ya Lobi Stars ya Nigeria (2-0), Nyasa Big Bullets ya Malawi (1-0) na USM Alger ya Algeria (2-1). Gor itarudiana na New Star mnamo Januari 20 mjini Douala, Cameroon.

Mshindi baada ya mikondo hii miwili ataingia mechi za makundi na kujihakikishia tuzo ya Sh27.9 milioni.

Rekodi ya Gor Mahia katika mashindano ya Afrika ugenini tangu mwaka 2009:

APR (Rwanda) 1-0 Gor (Februari 2009)

Ferroviario Maputo (Msumbiji) 3-0 Gor (Februari 18, 2012)

Anse Reunion (Ushelisheli) 0-5 Gor (Machi 2, 2013)

Bitam (Gabon) 1-0 Gor (Februari 16, 2014)

Esperance (Tunisia) 5-0 Gor (Machi 10, 2014)

CNaPS (Madagascar) 3-2 Gor (Machi 1, 2015)

AC Leopards (Congo Brazzaville) 1-0 Gor (Aprili 5, 2015)

CNaPS (Madagascar) 1-0 Gor (Februari 27, 2016)

Leone Vegetarianos (Equatorial Guinea) 1-1 Gor (Februari 21, 2018)

Esperance (Tunisia) 1-0 Gor (Machi 18, 2018)

Supersport United (Afrika Kusini) 2-1 Gor (Aprili 18, 2018)

Rayon Sport (Rwanda) 1-1 Gor (Mei 6, 2018)

Yanga (Tanzania) 2-3 Gor (Julai 29, 2018)

USM Alger 2-1 Gor (Agosti 29, 2018)

Nyasa Big Bullets (Malawi) 1-0 Gor (Desemba 5, 2018)

Lobi Stars (Nigeria) 2-0 Gor (Desemba 22, 2018)

New Star vs. Gor (?)

You can share this post!

MATHEKA: Idara husika ziwe na azma moja ya kumaliza ufisadi

ADAKA yawarai Wakenya kuzidisha vita dhidi ya pufya

adminleo