Habari za Kitaifa

Sababu za Jaji Mugambi kujiondoa kesini na kumsamehe Masengeli

Na RICHARD MUNGUTI September 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli sasa yuko huru.

Katika uamuzi wa kushtua aliyotoa Ijumaa Jaji Lawrence Mugambi alifutilia mbali hukumu na kifungo cha miezi sita aliyompa Bw Masengeli baada ya kubaini kuwa msamaha ambao afisa huyo aliwasilisha korti ulikuwa wa “ukweli”.

Vile vile, Jaji Mugambi alijiondoa kutoka kesi hiyo kutokana na kila alichotaja kama “sababu za kibinafsi”.

“Nia ya mahakama hii haikuwa kumwadhibu Bw Masengeli hivyo tu, bali kuhakikisha kuwa hukumu hiyo inarejesha hadhi ya Idara ya Mahakama…. Alihojiwa na mawakili. Ilibainika kuwa majibu yake yalionekana kama ya kweli,” jaji huyo akasema.

“Mahakama hii haina nia ya kumwadhibu mtu ambaye ameomba msamaha kwa njia ya haki,” Bw Mugambi akaongeza.

Jaji huyo aliwataka Wakenya wote kuheshimu uhuru wa mahakama na utawala wa kisheria

Baada ya Jaji Mugambi kujiondoa kutoka kwa kesi inayohusu kupotea kwa watu watatu waliotekwa nyara Kitengela mwezi jana na kupatikana Ijumaa eneo la Gachie, kaunti ya Kiambu, kesi hiyo iliwasilishwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome.

Sasa Jaji Mkuu atateua jopo la majaji watatu kuendelea na kesi hiyo.

“Suala hili ni lenye umuhimu mkubwa kwa umma na walalamishi wameibua masuala mazito kisheria yanayohitaji kusikizwa na jopo la majaji. Kwa hivyo, ninawasilisha kesi hii kwa Jaji Mkuu ili ateue majaji wa kuisikiza na mimi nisiwepo,” Jaji Mugambi.

Akiomba msamaha Bw Masengeli alisema anamheshimu Jaji huyo, mahakama hiyo na Idara ya Mahakama kwa ujumla.

Aliahidi kutii maagizo ya mahakama na mahitaji ya kikatiba.

“Naomba msamaha kwa mahakama hii kwa yale yaliyotokea na kuchangia kutolewa kwa maagizo haya. Mheshimiwa Jaji nakuheshimu kwa kazi mzuri unayofanya ya kuzingatia utawala wa kisheria. Kama afisa wa polisi ni wajibu wangu kuhakikisha kuwa maagizo ya mahakama yanaheshimiwa. Naomba radhi,” Masengeli akasema.

“Naomba kwamba mahakama hii ikubali ombi langu na kuniondolea hukumu na kifungo cha miezi sita,” akaeleza.

Akielekezwa na wakili wake Cecil Miller Masengeli alieleza kuwa alifeli kufika mahakamani kutokana na kuhusika kwake katika operesheni za kiusalama katika kaunti za  Lamu, Taita Taveta, Garissa na Wajir ambako kituo cha polisi kilishambuliwa na wapiganaji wenye silaha.

Bw Masengeli alieleza kuwa yeye ndiye anasimamia operesheni za mipakani na ilimbidi kuwepo wakati wa operesheni hizo na ndiposa akafeli kufika mahakamani alivyoagizwa.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga