Akili MaliMakala

Ufugaji wadudu wa BSF wapiga jeki ufugaji kuku

Na LABAAN SHABAAN September 21st, 2024 2 min read

KIJIJINI Nogirwet, eneo bunge la Chepalungu, Kaunti ya Bomet, wakulima wamekumbatia ubunifu kupunguza gharama ya chakula cha kuku kwa kufuga wadudu aina ya Black Soldier Flies (BSF).

Mtindo huu umewawezesha wafugaji wengi kuendesha ufugaji wa kuku kwa gharama nafuu.

Mintarafu hii, hali yao ya maisha imepigwa jeki wakiwa na imani ya kuwa na mfumo thabiti wa utoshelevu wa chakula.

Kundi la wakulima la Nogirwet Poultry and Maggot Farmers Community Based Organisation, chini ya uongozi wa Nicholas Rotich, kimekuwa mfano bora wa jinsi ufugaji wa BSF unavyoweza kusaidia wafugaji.

Chama hiki kina wanachama 50, wanawake 24 na wanaume 26. Kwa msaada wa Shirika la Red Cross, walipata kuku na wadudu aina ya BSF, ambao wamekuwa msaada mkubwa kwao.

“Red Cross ililenga kuhakikisha kuna chakula cha kutosha katika jamii hii na sisi tumekumbatia mradi kikamilifu,” alisema Rotich.

Katika sehemu ya juu ya Nogirwet, wakulima waliwezeshwa kufuga kuku, huku sehemu za chini zikisaidiwa kukumbatia kilimo cha umwagiliaji.

Wadudu wa BSF wakifungwa kwenye beseni ndani ya kivungulio Bomet. PICHA | LABAAN SHABAAN

Eneo hili lina nafasi ya kutosha kufugia kuku.

“Kuku hawa wanataga mayai tunayoyasambaza masokoni,” alisema Rotich.  “Sisi pia huuza kuku kwa wateja wa maeneo mbalimbali Bomet.”

Kwa lengo la kufaidika na mpango uliowekwa na Shirika la Red Cross, wakulima walijiunga na kuunda vikundi.

Walipewa chakula cha vifaranga na chakula cha kuku wakubwa kiasi bila malipo.

Ili kuboresha lishe, kundi hili huongeza mahindi, mboga, mtama, soya na kadhalika katika mseto wa lishe ya kuku wao.

Pia, huwaruhusu kuku kuzunguka huru ili wale wadudu kutoka kwenye mazingira.

Mwanachama wa Nogirwet Poultry and Maggot Farmers kaunti ya Bomet akionyesha kuku wanaofugwa kutumia BSF. PICHA | LABAAN SHABAAN

“BSF wana kiwango kikubwa cha protini muhimu sana kwa kuku na mayai yenye afya,” Rotich anasema,  “Hatupitii gharama kubwa ya kufuga BSF kwa sababu huwa tunakusanya taka za shamba na jikoni kuwalisha wadudu hawa.”

Wafugaji hawa wamejenga greenhouse kwa jitihada za pamoja za wanachama wa kikundi, wakitumia rasilimali walizokuwa nazo nyumbani mwao.

Kwa sasa, wao hutumia BSF kulisha maelfu ya kuku wanaofuga huku wakinuia kuuza kwa wingi siku za usoni.

Hata hivyo, kuna changamoto: Rotich anaeleza kuwa hawajafaulu kudhibiti joto wanapowafuga BSF katika kivungulio. Wadudu hawa huhitaji joto kati ya nyuzi joto 25 hadi 35.

“Hili eneo letu huwa na jua kali sana na hutuwia vigumu kudhibiti,” anafafanua Rotich. “Siku za usoni tutanunua neti ya kuweka kivuli chini ya greenhouse ili kupunguza joto.”

Pia, soko la bidhaa ya shughuli hii ya kilimobiashara huwa mbali katika maeneo ya Chebunyo na Sigor ambapo ili wao wafike, hutumia barabara mbovu.

Mwenyekiti wa Nogirwet Poultry and Maggot Farmers kaunti ya Bomet Nicholas Rotich akionyesha kuku wanaofugwa kutumia BSF. PICHA | LABAAN SHABAAN