Habari za Kitaifa

Gachagua: Nimemalizana na Ruto

Na CHARLES WASONGA September 21st, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa amefichua wazi kukatika kwa urafiki kati yake na bosi wake Rais William Ruto akiapa kuanzisha kampeni kote nchini kuelezea wafuasi wake sababu za kuvunjika kwa uhusiano huo.

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Ijumaa usiku, Septemba 20, 2024 Bw Gachagua alisema amekuwa akikosa kuhudhuria shughuli za Rais Ruto kwa sababu ya kutoalikwa.

“Huwa sipati habari kuhusu mikutano na shughuli za rais bila kupata mwaliko rasmi. Hii ni kwa sababu nilioondolewa kutoka ukumbi wa WhatsApp ambako ratiba za shughuli za rais huwekwa. Niliondolewa na Bw Maiyo ambaye ni Katibu wa Kibinafsi wa Rais. Ni kitendo cha kijinga,” akasema.

Bw Gachagua alisema kitendo hicho ni sehemu ya njama pana ya kumtenga na shughuli za serikali ili kumsawiri kama mkaidi na hatimaye atimuliwe afisini.

“Hii ndio maana mkutano ulifanyika juzi Nyahururu na mwingine ukafanyika katika makazi ya waziri mmoja mtaani Kitisuru ambako njama ya kuniondoa afisini ilipangwa. Hii sio siri,” Bw Gachagua akasema.

“Hii ndio maana nimepanga kukutana na wafuasi wangu kote nchini kuwaelezea kuhusu yale ninayopitia ili wajue kwani wao ndio walinichagua. Mkutano wa kwanza ulikuwa leo (Ijumaa) katika soko la Marikiti hapa Nairobi,” akaeleza.

Bw Gachagua alisema kuwekwa gizani kuhusu shughuli za Rais Ruto ndiko kulichangia yeye kutofika katika uwanja wa ndege wa JKIA, Jumapili iliyopita kumkaribisha kiongozi wa taifa alipowasili kutoka ziara ya Ujerumani.

Dkt Ruto alikaribishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na maafisa wengine wakuu serikalini.

“Sikuwa na habari kuhusu saa ambayo Rais angewasili. Na leo, Ijumaa, nimesikia ataelekea New York, Amerika lakini sijui anaondoka saa ngapi na hajaongea namu tangu asubuhi,” Bw Gachagua akasema.

Mnamo Jumapili wiki jana, Naibu Rais pia hakuhudhuria ibada iliyohudhuriwa na Rais Ruto katika Kanisa la African Independent Pentecostal Church of Afrika (AIPCA) katika ngome ya Gachagua mjini Nyeri.

Kiti kilichotengewa Naibu Rais kando ya kile cha Rais Ruto kilisalia wazi katika muda wote wa ibada hiyo.

Lakini kwenye mahojiano ya Ijumaa, Bw Gachagua alisema wakati huo alikuwa akihudhuria ibada nyingine katika kaunti jirani ya Kirinyaga.

“Sikujua saa ambayo Rais angewasili Nyeri na unajua kwamba kanuni ya kanisa Katoliki ni kwamba hauwezi kuondoka hadi ibada iishe,” akasema.

Bw Gachagua alilalamika wazi kwamba amekuwa akidhulumiwa na watu anaodai kuwa marafiki wa Dkt Ruto ilhali rais mwenyewe hachukui hatua zozote kuzuia vitendo hivyo.

Alimtaka Rais kuzingatia ahadi aliyotoa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kwamba atahakikisha kuwa naibu wake hadhulumiwi na kutishwa alivyofanyiwa wakati wa utawala wa rais mstaafu Bw Uhuru Kenyatta.

“Najua kwamba kuna ahadi ambazo Rais hajatimiza kutokana na hali ngumu ya kiuchumi. Lakini anapaswa kutimiza ahadi hii, isiyogharimu chochote, ya kuhakikisha kuwa naibu wake hatishwi na kudhulumiwa na wandani wake,” Bw Gachagua akaeleza.

Lakini licha ya kuelezea jinsi uhusiano kati yake na Rais Ruto umezorota, Bw Gachagua alishikilia kuwa hakuna hoja ya kumtimua afisini inaweza kuwasilishwa bungeni bila idhini ya bosi wake.