Gachagua: Nilitusiwa mara tano na afisa mkuu serikalini katika uwanja wa ndege
NAIBU Rais, Rigathi Gachagua analalamikia kudunishwa na baadhi ya viongozi serikalini na wandani wa Rais William Ruto wanaotofautiana naye kisera.
Kulingana na Bw Gachagua, hali imekuwa mbaya zaidi kiasi cha kurushiwa maneno mazito.
Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen mnamo Ijumaa jioni, Septemba 20, 2024, Naibu Rais alitaja kisa ambapo afisa mmoja mkuu serikalini alimtukana katika uwanja wa ndege ambao hakuufichua.
“Majuzi, afisa mmoja mkuu serikalini alinitukana mara tano katika uwanja wa ndege,” Bw Gachagua alisema.
Hata hivyo, hakufichua majina ya afisa huyo.
Naibu Rais analalamikia hadhi yake kudunishwa katika serikali aliyoshiriki kuunda 2022.
Anasema Ruto ndiye alimuandama na kumuomba awe mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa sababu alisimama naye kidete alipokuwa akihangaishwa na serikali ya Jubilee.
Alisema Dkt Ruto aliahidi familia yake; mkewe, Pasta Dorcas Gachagua na wanawe, kwamba hatampitishia madhila aliyopitia endapo angeibuka kidedea, katika kinyang’anyiro alichomenyamana na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.
Katika mahojiano ya Ijumaa, Bw Gachagua alionekana kuwa mwingi wa hasira kufuatia tetesi za kudunishwa kwenye serikali ya Kenya Kwanza.
Alisema, mambo yamezidi unga Rais Ruto akiendelea kusalia kimya licha ya baadhi ya viongozi kumrushia cheche za maneno kiongozi wa nchi akiwepo.
Katika siku za hivi karibuni, uhusiano wa Gachagua umeonakana kuwa na doa kiasi cha kukosa kuandamana na Rais kwenye hafla ambazo awali walikuwa wakiandamana sako kwa bako.
Alidai baada ya ‘handisheki’ kati ya Rais Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw Raila Odinga, kauli aliyopewa na Rais kuhusu ujio wa Odinga serikalini, imegeuka kuwa jukwaa la kutaka kumuondoa mamlakani.
Hata hivyo, alihoji hilo litatimia endapo bosi wake atapeana mwelekeo kwa bunge lipige kura za kukosa imani naye.
Bw Gachagua hakusita kudokeza kwamba ufa upo kati yake na Dkt Ruto.
Jumapili iliyopita, Septemba 15, 2024, naibu rais hakuandamana na bosi wake alipozuru Nyeri, eneo ambalo linakisiwa kuwa ngome ya Gachagua.
Badala yake, naibu rais alihudhuria ibada ya kanisa Kaunti ya Kirinyaga.
Kiongozi wa wengi Bunge la Kitaifa, Bw Kimani Ichung’wah, aliyeandamana na Rais Ruto alimtaka kiongozi wa nchi kuwaondoa serikalini baadhi ya viongozi wakuu aliodai wanalemaza jitihada za Rais kuhudumia wananchi.
Bw Ichung’wah alitumia jina ‘nyoka’, akiashiria viongozi hao japo hakuwataja kwa majina yao.
“Ukweli ni kwamba ninadunishwa na baadhi ya viongozi serikalini, ninahitaji heshima kama naibu rais wa Kenya,” Gachagua aliteta.
Aidha, anamtaka Rais Ruto kuweka ahadi ya maneno yake kwamba hatawahi kumdunisha naibu wake, ahadi alizotoa 2022 wakati akifanya kampeni kuingia Ikulu.
Dkt Ruto, wakati akihudumu kama naibu wa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye kwa sasa ni mstaafu, alilalamikia kutengwa na hata kudunishwa katika serikali aliyosaidia kuunda 2013 na kuiwezesha isalie mamlakani 2017.