Rais Ruto kukutana na polisi wa Kenya walioko Haiti kukabiliana na mgenge
RAIS William Ruto anatarajiwa kukutana na polisi wa Kenya walio Haiti kabla ya kuelekea New Yok kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Rais huyo alitoka nchini Ijumaa, Septemba 20, 2024.
Akizungumza na Taifa Jumapili, Godfrey Otunge, kamanda wa Ujumbe wa Kulinda Usalama wa Kimataifa (MSS) alisema wako tayari kumpokea Rais wakati wowote, na hivyo kuwa mara ya kwanza kwa Rais Ruto kusafiri nchini humo tangu aingie mamlakani 2022.
Hatua ya rais ya kusafiri hadi Porto-Au-Prince ni muhimu kwa sababu sehemu ya ajenda yake New York, ujumbe ulionyesha, itakuwa kujadili ustawi wa MSS, ambayo mkataba wake unamalizika mwezi ujao lakini unatarajiwa kufanywa upya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili uendelee kwa muda wa mwaka mmoja.
“Rais atazungumza na maafisa waliojitolea kuhakikisha kwamba amani inarejeshwa hapa Haiti,” alisema.
Timu ya mawasiliano ya Baraza la Mpito la Rais la Haiti ilisema kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.
“Ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili; kati ya Jamhuri ya Haiti na Kenya, kwa kutilia mkazo zaidi ushirikiano katika masuala ya usalama na maendeleo,” taarifa ya timu hiyo ilisoma.
Ilisema zaidi kwamba Bw Edgard Le-Blanc Fils ambaye ni mkuu wa Baraza la Mpito la Urais nchini Haiti ambalo lilikubali maafisa wa Kenya watumwe Haiti atajadiliana na rais kuhusu masuala ya kimataifa.
Timu ya mawasiliano ilisema kwamba itafichua maelezo zaidi ya ziara hiyo kwa wakati ufaao.
Rais Ruto aliondoka nchini na anatarajiwa kushiriki katika kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York.
Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya maafisa wa Kenya pamoja na wale Haiti kuwakamata viongozi wawili wa magenge.