Habari za Kitaifa

Kahiga, Abdullahi waelezea sera zao kura ya CoG ikinukia

Na JUSTUS OCHIENG’ September 22nd, 2024 2 min read

MAGAVANA wawili ambao wametangaza kuwa wanamezea mate uenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (CoG) wameelezea maono yao ambayo wanasema yatasaidia kufanikisha ugatuzi nchini.

Uchaguzi wa CoG utakuwa ukiandaliwa mnamo Oktoba 7 wakati ambapo mrithi wa mshikilizi wa afisi hiyo kwa sasa Anne Waiguru atakuwa akisakwa.

Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi (ODM) na mwenzake wa Nyeri Mutahi Kahiga (UDA) wamesema kuwa watapigania pesa kutolewa mapema kwenye kaunti kama sehemu ya kutetea ugatuzi.

Pia, watahakikisha majukumu yote yanayostahili kugatuliwa yanapewa kaunti kuzisimamia kuipa nguvu utawala huo ambao ulikumbatiwa kufuatia kurasimishwa kwa Katiba ya 2010.

Bw Abdullahi alisema kaunti zimekuwa zikipokea pesa kwa kuchelewa, hilo likiwa na mchango hasi katika utoaji wa huduma kwa Wakenya.

“Naamini kuwa sasa tuna waziri mpya wa Fedha (John Mbadi) ambaye ni mtu anatathmini hali na hujali kaunti. Atahakikisha fedha zinafikia kaunti kwa wakati ili huduma zisitatizike,” akasema Abdullahi kwenye mahojiano na Taifa Dijitali.

Gavana huyo alisema kuwa kaunti zikipokea pesa kwa wakati, basi uchumi utaimarika na kutakuwa na mapato mengi ya kutozwa ushuru na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA).

“Ukichelewa kulipa wafanyakazi huwa inaathiri pesa ambazo zinaelekezwa kwa KRA pamoja na pensheni. Kuchelewa kuwalipa wawasilishaji wa bidhaa pia huathiri uchumi wa kaunti mbalimbali,” akasema Bw Abdullahi.

Bw Kahiga naye alisema kuwa suala la kuhakikisha kuwa uwepo wa CoG unawekwa kwenye sheria litapewa kipaumbele.

Hii itahakikisha kuwa magavana wanasukuma ajenda za kaunti kwa msingi wa kisheria.

“CoG kwa sasa haijawekwa kwenye sheria na hilo ni jambo ambalo linastahili kuangaliwa kwa makini. Ugatuzi umechukua miaka 11 tangu uanzishwe ilhali bado kuna majukumu ambayo hayapo kwa kaunti,” akasema Bw Kahiga.

Bw Abdullahi ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa CoG alisema kuwa kuna haja ya kuharakisha kuhamishwa kwa majukumu yote ya ugatuzi hadi kaunti kwa mujibu wa sheria.

“Hili ni suala ambalo tumelizungumzia mara kadhaa kwa kuwa kuna majukumu zaidi ya 500 ambayo yamegatuliwa lakini bado kaunti hazijisimamii. Majukumu haya yana thamani ya Sh270 bilioni,” akasema gavana huyo wa Wajir.

“Ukweli ni kuwa kazi nyingi imefanywa na tutasukuma kuhakikisha kuwa wajibu ambao umesalia unatekelezwa ili kaunti isimamie majukumu yake,” akaongeza Bw Abdullahi.

Bw Kahiga aliendelea kumimina ahadi akitoa makataa ya mwaka mmoja kuhakikisha kuwa majukumu yote ambayo bado yapo kwenye serikali kuu na yanastahili kuwa katika kaunti, yanahamishwa.

“Nitahakikisha kuwa mawaziri wa kaunti wanashauriana na wenzao kutoka serikali kuu kuhusu usimamizi. Pia, uhusiano kati ya serikali kuu na kaunti unastahili kuwa ule ambao kila mrengo unafanya kazi yake na pesa zinawasilishwa kwa wakati,” akaongeza.

Kinyanganyiro cha ugavana kati ya Bw Kahiga wa UDA na Bw Abdullahi wa ODM kumefasiriwa kama vita vya ubabe kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua dhidi ya ushirikiano wa Rais William Ruto na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga.