Habari za Kitaifa

Mitambo ya kusafisha maji kuwafaa wanafunzi

Na KALUME KAZUNGU September 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imezindua mikakati ya kuweka mitambo ya kusafisha maji kwa matumizi shuleni.

Shule kadhaa, ikiwemo Wiyoni kisiwani Lamu na zile za maeneo ya nchi kavu, hasa Mokowe, tayari zimenufaika na mpango huo unaolenga kuhakikisha wanafunzi hawatatiziki kupata maji safi.

Akihutubu wakati wa ufunguzi wa mtambo wa kusafisha maji katika Shule ya Wiyoni mnamo Jumamosi, Septemba 21, 2024 Gavana wa Lamu, Issa Timamy, alisema utawala wake utashirikiana kwa karibu na wahisani kuhakikisha mpango huo unafanikishwa kwenye taasisi nyingi za elimu eneo hilo.

Mpango huo ulidhaminiwa na shirika la kibinafsi la Helping Hand kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Lamu.

“Haya yote tunayatekeleza kuzuia mateso miongoni mwa wanafunzi wakitafuta maji wakati wanapaswa kusalia madarasani kusoma,” akasema Bw Timamy.

Aliongeza, “Utawala wangu utajitahidi kuwakaribisha wahisani zaidi wenye moyo wa kusaidia wanafunzi na jamii yetu kwa jumla.”

Baadhi ya wakazi, wakiwemo wazazi waliohudhuria hafla hiyo, waliipongeza Serikali ya Kaunti ya Lamu na wahisani kwa jitihada zao katika kushughulikia uhaba wa maji miongoni mwa wanafunzi shuleni.

Bi Amina Athman, mkazi wa Wiyoni, alisema mbali na mtambo huo kusuluhisha tatizo sugu la uhaba wa maji shuleni, jamii zinazoishi karibu na shule hiyo pia zitanufaika.

Gavana wa Lamu, Issa Timamy (mwenye kanzu nyeupe-katikati) akiwa na maafisa wa shirika la Helping Hand wakati wa hafla ya uzinduzi wa mtambo kusafisha maji na kuyabadilisha kuwa safi kwenye shule ya Wiyoni, kisiwani Lamu mnamo Jumamosi, Septemba 21, 2024. PICHA|KALUME KAZUNGU

“Twajua mgeni akija mwenyeji hupona. Tunatarajia ujio wa mtambo huu pia utatunufaisha na sisi wanajamii kwa kiwango fulani,” akasema Bi Athman.

Wakati huo huo, wazazi katika shule zipatikanazo maeneo kame na yanayokumbwa na changamoto za uhaba wa maji wameisihi serikali ya kaunti, ile ya kitaifa na wahisani kuwapa kipaumbele katika ujenzi na uzinduzi wa mitambo aina hiyo.

Wazazi wa maeneo husika wamelalamika kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikosa kwenda shuleni wakilazimika kuandamana na wazazi wao hadi maeneo ya mbali kutafuta maji na chakula.

Bw Ahmed Islam, mkazi wa Ishakani mpakani mwa Kenya na Somalia, anasema wengi wao wamelazimika kuwahamisha watoto wao kutoka shule ya Ishakani hadi Kiunga kutokana na changamoto tele zinazokabili na kuandama eneo hilo, ikiwemo uhaba wa maji na chakula.

“Wahusika wazingatie maeneo ambayo ni dhahiri yanakabiliwa na uhaba wa maji kama hapa Ishakani, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe, Pandanguo, Witu, Bar’goni, Hindi na kwingineko,” akasema Bw Islam.

Sehemu kubwa ya Lamu hasa visiwani hukumbwa na uhaba wa maji safi.

Baadhi ya makazi yaliyo na visima bado hutatizika kwa kuwa maji yanayotoka visimani huwa na chumvi tele kwa kiasi ambacho ni vigumu kutumiwa kwa mahitaji muhimu ya nyumbani kama vile kunywa na hata kupikia.