Habari za Kitaifa

Katibu Omollo ataka wazazi kusaidia kuzima ghasia shuleni

Na GEORGE ODIWUOR September 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Masuala ya Ndani imewataka wazazi kusaidia serikali kudhibiti matukio ya ghasia shuleni.

Katibu wa wizara hiyo Dkt Raymond Omollo alisema kuna mtindo nchini ambapo visa vya mioto na ghasia vinaripotiwa katika shule tofauti katika muhula wa tatu.

Alisema baadhi ya mioto huanzishwa na watoto wachache wasio na nidhamu.

“Kumekuwa na wasiwasi kwamba tunapofika muhula wa tatu wakati wanafunzi wanakaribia kufanya mitihani, tunashuhudia visa vya utovu wa nidhamu na wanafunzi wachache hutumia fursa hii kuvuruga masomo,” Dkt Omollo alisema.

Alitoa changamoto kwa wazazi kuchukua jukumu la kuwashauri watoto wao kuwa raia wanaowajibika, wasishiriki katika visa vya uchomaji moto shuleni.

Alisema wazazi wanapaswa kuwaelekeza watoto wao katika njia sahihi ili waweze kufanikiwa kimaisha na kuepuka kwenda jela kwa kuvunja sheria.

“Wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wao wanakua na kuwa watu wa maana. Wazazi wapigane na utovu wa nidhamu miongoni mwa watoto,” alisema.

Wito wa Dkt Omollo kwa wazazi unajiri huku Wakenya wakisubiri ripoti kuhusu kilichosababisha moto katika shule ya Hillside Endarasha Academy katika Kaunti ya Nyeri uliosababisha vifo vya wavulana 21.

Visa vingine vya moto vimeripotiwa katika shule zingine kote nchini.