Habari za Kitaifa

Mbunge wa UDA azomewa na umati alipomshambulia Gachagua


MBUNGE wa Keiyo Kaskazini Adams Kipsanai alizomewa na wananchi alipojaribu kumkosoa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwenye mashindano ya soka katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Bw Kipsanai alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria fainali za Kombe la Gavana wa Elgeyo Marakwet katika uwanja wa Iten, ambapo wazungumzaji walimtaka Rais William Ruto na naibu wake kuzika tofauti zao na kuzingatia kufanikisha ajenda ya maendeleo waliyoahidi Wakenya wakati wa uchaguzi.

Wazungumzaji walihimiza maridhiano, wakiwataka viongozi hao wawili wakuu wa taifa kuacha kuzozana hadharani na kutafuta njia ya kuzika tofauti zao.

“Si vyema kwa viongozi wakuu wa serikali kushambuliana hadharani. Jambo la busara ni kuketi pamoja na kutatua shida zao faraghani ili kupata heshima ya watu wanaowaongoza,” Gavana wa Baringo Benjamin Cheboi alisema huku akimtaka Rais na naibu wake kutatua tofauti zao.

Jaribio la Bw Kipsanai la kumkosoa Bw Gachagua lilizimwa na kelele kutoka kwa umma.

“Bw Gachagua anapaswa kwenda polepole ….” alianza kusema, lakini kabla hajamaliza kauli yake umati ulimfokea ukisema Gachagua pia ni wetu (Gachagua pia ni kiongozi wetu.)

Hata hivyo waliozungumza walisisitiza umuhimu wa kuwaheshimu walio  mamlakani huku wakisema kuwa urais ni ishara ya umoja wa kitaifa na wanaorushiana matusi kwenye ofisi hiyo lazima wakome.

“Kila kiongozi lazima aheshimu wakubwa. Bila kujali hali, urais lazima uheshimiwe,” alisema Gavana wa Baringo, ambaye alisikitika kwamba viongozi wakuu wa serikali walikuwa wakikemeana waziwazi badala ya kukaa pamoja kusuluhisha tofauti zao.

“Hatupaswi kuwa na chuki za kisiasa. Badala yake, tuangazie ajenda ya maendeleo tuliyoahidi Wakenya,” akasema.

Ujumbe huo uliungwa mkono na viongozi wengine wa kisiasa waliokuwepo.

“Kama viongozi, lazima tukumbatie amani kwa mustakabali wa nchi yetu na kuheshimiana bila kujali tofauti zetu za kisiasa,” alisema Mbunge wa Marakwet Magharibi Timothy Kipchumba, ambaye aliwataka viongozi wote kukumbatia umoja kwa ustawi wa nchi.

Gavana wa Elgeyo Marakwet Wisley Rotich pia aliwataka viongozi wote kuungana kwa ajili ya nchi na maendeleo.

Bw Rotich aliwaambia viongozi kuacha siasa  kila siku na kuelekeza nguvu zao kwenye maendeleo ili kutimiza ahadi zao za uchaguzi kwa Wakenya.

“Tunapaswa kuacha siasa  ambazo zinaweza kusababisha migawanyiko miongoni mwa Wakenya. Tuzingatie siasa za maendeleo na tuepuke siasa za kuturudisha nyuma kwa vyovyote vile,” akasema Gavana wa Elgeyo Marakwet.