Makala

Kitendawili cha mshukiwa wa ajira feki za ng’ambo kuwa katika ziara ya Ruto nchini Ujerumani

Na SIMON CIURI, BENSON MATHEKA September 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

JINA la Ceaser Wagicheru Kingori almaarufu ‘mjanja’ lilijitokeza kwa mara ya kwanza mnamo Agosti mwaka jana wakati wa uchunguzi kuhusu utapeli wa ajira wa kima cha Sh600 milioni unaohusishwa na kasisi mmoja jijini Nairobi.

Wakati huo, uchunguzi huo ulilenga Bw James Wanjohi wa Kanisa la Jesus Culture Ministries ambaye alilaumiwa kwa kukusanya mamilioni ya pesa kutoka kwa maelfu ya watu wanaotafuta kazi  ng’ambo ambazo hazikupatikana.

Wale waliotapeliwa walimlipa Bw Wanjohi ada ya kati ya Sh100, 000 na Sh140, 000 kwa kila mtu- walipigwa marufuku wakati wa kuomba viza katika Ubalozi wa Canada nchini Kenya baada ya maombi yao kupatikana kuwa na habari za uwongo.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imewasilisha faili kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) zinazopendekeza Bw Wanjohi ashtakiwe pamoja na mshukiwa mwingine, Bw Alphonse Kioko wa kampuni ya Amble Beginning Consult, ambaye pia anashtakiwa kwa kuwalaghai maelfu ya wanaotafuta kazi Sh890 milioni.

Wakati wa uchunguzi wa Taifa Leo, kulikuwa pia na malalamishi dhidi ya Bw Kingori, ambaye wakati huo alikuwa mwajiri chipukizi, lakini waathiriwa wake wengi waliojitokeza walikataa mahojiano wakitaja ahadi kwamba wangerejeshewa pesa.

Hata hivyo, hawakurudishiwa pesa zao na malalamishi dhidi ya Bw Kingori na kampuni yake ya Vintmark Travel Agency Ltd, yamekuwa yakiongezeka katika DCI.

Vintmark Travel Agency Ltd inahudumu kutoka jumba la Kenindia kwenye barabara ya Loita katikati mwa jiji la Nairobi.

Taifa Leo imepitia maelfu ya taarifa za mashahidi zilizowasilishwa katika ofisi za DCI Nairobi na Wakenya na raia wa wageni wanaolalamika kuwa wamepoteza kwa pamoja karibu Sh720 milioni baada ya kuamini mikakati ya utapeli ya kampuni hiyo kupitia Tiktok na mitandao mingine ya kijamii kwa kazi za ng’ambo ambazo hawajawahi kupata.

Katika ulimwengu wa mashirika ya uajiri, Bw Kingori anafahamika kwa jina ‘mjanja’, labda kutokana na weledi wake wa kujiweka karibu na wenye ushawishi wa kimamlaka na kulinda maslahi yake ya kibiashara.

Ijapokuwa Bw Kingori hakuwa miongoni wa wajumbe wa serikali walioandamana na Rais William Ruto hadi Ujerumani kutia saini mikataba ya wafanyikazi, alipata njia yake kufika Berlin wakati wa ziara ya Rais mnamo Septemba 13 na 14.

Bw Kingori alipiga picha na waziri wa Leba Alfred Mutua wakati wa kutia saini Mkataba wa Ushirikiano wa Uhamiaji wa Wafanyakazi kati ya Kenya na Ujerumani.

Kando na Dkt Mutua, wengine walioandamana na Rais ni Mkuu wa Waziri Musalia Mudavadi na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye ni mgombeaji wa Kenya wa kiti cha uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Alipokuwa akijumuika na viongozi wa Kenya katika mikutano nchini Ujerumani kuhusu ajira ng’ambo, alikuwa ameacha orodha ndefu ya wahasiriwa wa hila na utapeli nchini Kenya ambapo wapelelezi walimwita kuhojiwa na wanalalamika kuwa hagusiki.

”Imefikia hatua sasa ambapo Bw Kingori amekuwa mgumu. Alipoitwa wiki iliyopita na mpelelezi kurekodi taarifa zaidi baada ya kundi jingine kuibuka likidai kuwa kampuni ya Vintmark Tours Travel Ltd imewalaghai, alimjibu afisa wa uchunguzi kuwa alikuwa Ujerumani. Alimtumia  picha yake akiwa na waziri,” Bw Njeru Nthigah, afisa wa Uchunguzi wa Jinai eneo la  Nairobi aliambia Taifa Leo katika mahojiano wiki jana.

“Ninapanga kukutana na Waziri Mutua na kumweleza jinsi utapeli umekita mizizi katika mashirika ya kuajiri na hatua ambazo zinafaa kutekelezwa kwa kasi kwa sababu hali hiyo inatia wasiwasi,” Bw Nthigah aliongeza.

Tulipowasiliana naye, Dkt Mutua aliambia Taifa Leo kwamba maajenti wengi wa mashirika ya ajira waliokuwa sehemu ya ujumbe huo nchini Ujerumani walilipa tikiti zao baada ya kuwasilisha ombi kwa serikali.

“Maajenti wengi wa uajiri walisafiri hadi Berlin kushuhudia kutiwa saini kwa makubaliano ya kazi ya nchi mbili na kuunganishwa na makampuni ya ajira ya Ujerumani. Kwa wale waliotuomba pia kuwa Berlin na kufanya, tuliwaambia ni sawa. Maajenti hao wote walilipa tiketi zao wenyewe. Maajenti waliosafiri kwa ndege kutoka Kenya au wanaoishi Ujerumani walikuwa zaidi ya 50,” Dkt Mutua alieleza.

Aliahidi kuchunguza suala la Vintmark Travel Agency Ltd na malalalamishi mengi ya udanganyifu.

Baada ya ziara hiyo ya Berlin, kampuni ya Bw Kingori ilichapisha nafasi za kazi nchini Ujerumani ikinukuu agizo la Rais.

“Kenya imetia saini mkataba wa kuruhusu Wakenya 250,000 wenye ujuzi kufanya kazi nchini Ujerumani. Wacha tutimize ndoto zako za kusafiri nje ya nchi kufanya kazi, kusoma, kuishi, kutembelea au kusafiri, huduma zetu ni pamoja na ombi la visa, tiketi za ndege, utafutaji wa kazi na pasipoti. Wacha tuanze mchakato wako wa kutuma maombi leo,” Vintmark Travel Agency Ltd ilichapisha kwenye Instagram.

Taarifa za walalamishi zinaonyesha waathiriwa wanaodai kutapeliwa na kampuni hiyo wanatoka mataifa kadhaa ya Afrika ikiwemo Kenya, Afrika Kusini na Congo.