Habari za Kitaifa

Kamata kamata ya viongozi wa Uasu yatia hasira wanafunzi wa vyuo; watishia kuingia barabarani

Na WAANDISHI WETU September 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI 20 wa Chama cha Kutetea Maslahi ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Nchini (UASU) na kile cha kutetea maslahi ya wafanyakazi wengine wa taasisi hizo (Kusu) walikamatwa jana walipokuwa wakiwasilisha malalamishi kuhusu mgomo wao bungeni na makao makuu ya wizara ya elimu.

Viongozi hao walikamatwa karibu na jumba la Jogoo, jijini Nairobi baada ya wao kuwasilisha taarifa yenye malalamishi yao bungeni wakielekea kwa afisa za Waziri wa Fedha John Mbadi na mwenzake wa Elimu Julius Ogamba.

Fujo zilitokea baada ya polisi kurusha vitoza machozi kwa wanachama wa UASU na KUSU waliokuwa wakiandamana kwa amani kuelezea matakwa yao.

Hayo yanajiri baada ya mgomo wao, ambao umesambaratisha shughuli za masomo katika vyuo vikuu vya umma, kuingia wiki yake ya pili.

Huku hayo yakijiri, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pwani kilichoko Kaunti ya Kilifi wametishia kujiunga na mgomo unaoendelea wa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu kitaifa.

Wanachama wa Muungano wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) na Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini (KUSU) wamekuwa katika mgomo kwa karibu wiki moja sasa, wakilalamikia serikali itekeleze makubaliano yao ya pamoja kuhusu nyongeza ya mishahara, kucheleweshwa kwa mishahara, miongoni mwa mengine.

Wanafunzi sasa wamesema wao pia wataingia kwenye maandamano pamoja na wahadhiri ili kudai haki yao ya kupata elimu iwapo serikali itashindwa kushughulikia matakwa ya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu yaliyo kwenye Makubaliano ya Pamoja (CBA) ya 2021-2025.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pwani (PUSA), Vincent Obondo, alisema hawataruhusu wanafunzi kuendelea kukaa vyuoni bila masomo kuendelea kutokana na mgomo huo.

Hata hivyo, serikali haijaonyesha dalili kwamba inalenga kuingilia kati kwa kushughulikia matakwa ya wafanyakazi hao.

Wahadhiri wanalalamikia hatua ya serikali kuchelewesha utekelezaji wa yaliyomo kwenye Mkataba wa Maelewano (CBA) wa 2021- 2025.

Viongozi wa Kusu pia wanataka marupurupu ya wafanyakazi wa vyuo vikuu, wasio wahadhiri, yasawazishwe na wapewe bima bora ya matibabu.

Athari za mgomo huo tayari zinaonekana kutokana na hali kwamba wanafunzi wanakaa tu vyuoni bila kusomeshwa.

Jana, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pwani walitishia kuungana na wahadhiri wao katika mgomo wakitaka wapewe haki yao ya kufundishwa huku wakiitaka serikali kutimiza matakwa ya wanachama wa UASU.

“Ikiwa wahadhiri wataendelea na mgomo, basi nasi tutagoma kuitisha haki yetu ya elimu. Sio vizuri kwa wanafunzi kukaa bila kufundishwa kwa muda wa wiki mbili ilhali walilipa karo,” akasema Vincent Obondo ambaye ni Rais wa Muungano wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pwani (PUSA).

Ripoti ya Hillary Kimuyu, Elizabeth Ojina, Maureen Ongala na Wachira Mwangi