Habari za Kitaifa

KIGEUGEU? Ruto sasa asifu Ford Foundation aliyoiponda majuzi kwa kufadhili maandamano

Na DANIEL OGETTA September 24th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto Jumanne Septemba 24, 2024 alikutana na Rais wa Wakfu wa Ford Foundation Darren Walker katika kile kinachoonekana kama hatua ya kurekebisha uhusiano uliovunjika alipolaumu shirika hilo la Amerika kwa kufadhili maandamano ya vijana dhidi ya Serikali yake.

Dkt Ruto, ambaye yuko Amerika kwa Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa, alisisitiza Kenya inathamini kujitolea kwa wakfu huo kulinda demokrasia.

“Kenya inathamini kujitolea kwa Ford Foundation kuunga mkono wito wa Kenya wa mageuzi katika taasisi za kiuchumi, hali ya hewa na teknolojia ya kisasa,” Rais Ruto alichapisha kwenye anwani yake ya X, bila kufichua maelezo zaidi.

Wakati wa maandamano ya Gen Z, Rais Ruto alionya shirika hilo akililaumu kwa kufadhili uasi dhidi ya serikali yake.

“Kenya ni nchi ya kidemokrasia inayoongozwa na utawala wa sheria na kusimamiwa na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia. Hatuwezi kuendesha nchi yetu kwa machafuko au mapinduzi. Tutahakikisha kuwa yeyote anayefadhili maandamano hayo atachukuliwa hatua za sheria,” akasema Rais Ruto akiwa Keringet, Kuresoi Kusini, Kaunti ya Nakuru.

“Tunataka Ford Foundation iwaeleze Wakenya jukumu lake katika maandamano ya hivi majuzi. Iwapo (Ford Foundation) hawapendezwi na demokrasia nchini Kenya, wanapaswa kujipanga au kuondoka. Tutawataja wote wanaopania kurudisha nyuma demokrasia yetu tuliyopata kwa bidii,” Dkt Ruto aliongeza.