Makala

Alitibua mpango ya ‘kumuuza’ kwa jibaba tajiri, sasa balozi wa elimu ya mtoto wa kike

Na LEAH MAKENA September 27th, 2024 3 min read

KATIKA tambarare za kusini mwa Kenya, leso nyekundu za Wamaasai zimepamba kila mahali. Hapa, tunakutana Sianto Nashipae, ambaye amekuwa nembo ya ustahimilivu na ukakamavu.

Safari ya kutia moyo ya Nashipae ilianza katika kijiji kidogo cha mpakani mwa Kenya na Tanzania, alikozaliwa na kulelewa.

Kama wasichana wengi kwenye jamii yake ya Maa, hatima yake ilionekana kuamuliwa mapema kwa sababu alipofika umri wa miaka 13, aliozwa kwa mzee mmoja kwenye jina tajika. Utajiri wake wa mifugo wengi ulimaanisha kwamba angeilipa familia ya Nashipae kiasi kizuri cha mahari, hivyo kujitwalia mwanamwali, msichana mbichi – Sianto Nashipae.

Kulingana na desturi, ndoa ya Nashipae ilipangwa bila kumhusisha na masomo yake yalikatizwa ghafla ili aandaliwe kwa maisha mapya ya kuwa mke wa mtu.

“Ndoto zangu za kuwa mwalimu zilikatizwa ghafla kwani nilifanyiwa kikao na kutakiwa kuacha shule ili niandaliwe kwa majukumu ya maisha mapya ya kuwa mke na mama,” alieleza Nashipae.

Kadri siku yake ya kufunga pingu za maisha ilipokaribia, Nashipae alizidi kujawa na wasiwasi asijue la kufanya kwa sababu alikuwa ameshuhudia ndoto za wasichana wenzake zikizimwa kutokana na ndoa za mapema.

Kupitia usaidizi wa mwalimu mmoja kijijini aliyetambua hofu yake, Nishipae alitambulishwa kwa shirika moja lisilo la kiserikali lililokuwa likinusuru wasichana waliokuwa wakikimbia ndoa za mapema.

Hapo ndipo alitoroka siku chache kabla ya harusi yake na kukimbilia kwa afisi ya shirika hilo.

“Moyoni mwangu, nilikuwa na tamanio tofauti, tamanio la kupata fursa ya kuendeleza masomo ili ninyooshe njia ya maisha yangu. Nilipopata mwanya wa kuhepa, nilitorokea kwenye jamii mpya nilikopata wasichana wadogo kama mimi waliokuwa na kiu ya elimu,” Nashipae anasimulia.

Sianto Nashipae aliyeponyoka ndoa ya mapema, sasa ni balozi wa elimu ya mtoto wa kike katika jamii yake ya Maasai. Picha|Leah Makena

Binti huyo anaeleza jinsi alirejelea safari yake ya elimu baada ya kupata ufadhili.

Yeye na wasichana wenzake walijizatatiti kwa hali na mali kwani kila mmoja wao alitamani kufua dafu kwenye masomo.

Anakumbuka jinsi wafadhili wao walivyofuatilia mienendo yao ili wasijipate tena kwenye mikono ya waliotaka waolewe mapema.

Nashipae anasema kuwa ijapokuwa aliwakosa wazazi na ndugu zake kwa muda, alijikaza ili asijipate kwenye mikono ya bwenyenye aliyekuwa akimmezea mate.

“Tulitia fora na tukafanya vyema sana kwenye masomo. Ijapokuwa tulikuwa mbali na familia zetu, tuliamini kuwa ipo siku tungekutana nao tukiwa wasomi tayari kubadilisha jamii zetu,” Nashipae alieleza.

Kwa sasa, Nashipae, 21, ni mwanga kwa wasichana wadogo kwenye jamii ya Maa na ametoa changamoto kwa wazazi wengi kukoma kusukuma binti zao kwenye ndoa za mapema na badala yake kuwapa elimu.

Safari yake imewatia wanajamii na viongozi moyo na wengi wamebadilisha mwenendo kwa kuhakikisha kuwa binti zao wadogo wamepata elimu.

Aliyekuwa mzee wa mtaa yapata miaka mitano iliyopita, Olumisi Lemuani anakiri kuwa Nashipae na baadhi ya wasichana wengine wamebadilisha mtazamo wa wazazi wengi kwani sasa binti wengi wanapata fursa ya kusoma bila kusukumwa kwenye ndoa za mapema.

“Msichana huyu na wenzake wamefanikiwa katika kushawishi jamii yetu kuwa kuna ubora wa kutuma mtoto wa kike shuleni badala ya kumuoza mapema kwa lengo la kupata mali inayoisha upesi mno,” anasema Lemuani.

Nashipae amekamilisha masomo ya shule ya upili na sasa anafanya shahada ya Afya ya Jamii. Ndoto yake ya kuwa mwalimu ilibadilika kuwa lengo pana, kuelimisha jamii kuhusu hatari ya ndoa za mapema na umuhimu wa kupiga mabinti jeki kwenye masomo.

“Niliamua kuwa ‘mwalimu’ wa jamii kupitia kozi yangu ili niweze kuwa mtetezi wa mtoto wa kike na nielimishe wazazi wengi kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu ya binti zao,” alieleza Nashipae.

Mara kwa mara, binti huyu hurudi kijijini kama kiongozi anakofanya vikao na wazazi na kueleza wasichana wadogo kuhusu haki zao. Amekuwa ishara ya tumaini na mabadiliko na amethibitisha kuwa yeyote anaweza kuvunja minyororo ya mila na kuafikia malengo yake kwenye maisha.

Kutokana na ukakamavu wake, Nashipae amebadilisha maisha yake na ya wasichana wengi wa jamii ya Maa, hadithi inayotia wengi motisha na kuwapa kila sababu ya kutimiza ndoto zao.