Wananchi watakiwa kupanga uzazi ili kuzima umaskini
VIONGOZI katika Kaunti ya Kwale wamewataka wakazi kuzingatia upangaji uzazi kama njia ya kupunguza umaskini katika kaunti hiyo.
Naibu Gavana, Bw Chirema Kombo, alisema familia ambazo wazazi hawajazingatia mfumo huo, zinachangia katika kuendeleza umaskini.
Akizungumza akiwa Samburu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mpango wa Uzazi Duniani (Contraceptive Day) Jumamosi, Bw Kombo alisema kuwa familia zilizopangwa zitawezesha wazazi kutoa mahitaji ya kutosha kwa watoto wao katika afya na elimu.
“Tunafahamu kwamba kuna viwango vya juu vya umaskini miongoni mwa baadhi ya jamii zetu. Wazazi wanapaswa kuelewa kuwa upangaji uzazi si kuhusu kupunguza idadi ya watoto lakini pia kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji ya msingi ipasavyo,” alisema Bw Kombo.
Aliwarai wazazi kuchukua muda wa kutosha kuwalea watoto kabla kuongeza idadi yao.
Bw Kombo alisema kuwa familia zilizopangwa vizuri huwezesha wazazi kugawa rasilimali za kutosha kwa kila mtoto, kuboresha viwango vya maisha yao na kuhakikisha kuwa wanapata elimu ipasavyo.
Kwale ni kati ya kaunti zenye viwango vya chini vya matumizi ya njia za kupanga uzazi kutokana na dhana potofu zinazozunguka suala hilo kama vile utamaduni wa jamii na maswala ya kidini ambayo yamekuwa vikwazo kubwa.
Bw Kombo aliwataka viongozi wa jamii, wahudumu wa afya, na mashirika ya kuendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kupanga uzazu na kuondoa dhana potofu zinazochangia unyanyapaa unaozunguka suala hilo.