Makala

Kocha wa kandanda alivyonyemelea wavulana kutoka familia maskini na kuwachafua kimapenzi

Na MAUREEN ONGALA October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA wa timu ya kandanda ya wavulana wa chini ya umri wa 15 mjini Malindi, Patrick Mbauni Murithi, almaarufu kama Coach au Daddy, huenda akatumikia kifungo jela baada ya kupatikana na hatia ya kulawiti watoto na utengenezaji video chafu za watoto.

Mmiliki huyo wa Klabu ya Soka ya Patarv, alipatikana na hatia mnamo Septemba 25 mwaka huu.

Wapelelezi walimkamata mnamo Novemba 2023 katika mji wa Malindi.

Murithi alifikishwa katika Mahakama ya Malindi na kushtakiwa kwa makosa 10 ya ulawiti kufanya vitendo vichafu na mtoto, ponografia ya watoto na ulanguzi wa wavulana wanne.

Mshtakiwa alitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Agosti 1, 2022, na Januari 11, 2023, katika makazi yake ya kukodi ya Mwembe Tayari eneo la Kisumu Ndogo mjini Malindi.

Kufikia wakati wa kukamatwa, wapelelezi walipata wavulana wanne wenye umri wa kati ya miaka tisa hadi 16 ndani ya nyumba hiyo.

Kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani, Bw Murithi angewaingiza wavulana hao kwenye timu yake na kuwapa wao na baadhi ya wanafamilia wao elimu, msaada wa kifedha na mengine.

Familia hizi zilimwamini na mara nyingi zilimruhusu kuishi na wavulana hao, wakiamini kwamba alikuwa akiwafundisha kandanda ipasavyo.

Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa angewanyanyasa kingono na kurekodi vitendo hivyo viovu kwenye simu yake ya mkononi.

Mshtakiwa alijitetea akisema kuwa, aliwapa malazi wavulana ambao wazazi wao walikuwa wakipitia matatizo ya kifedha.

Alikiri kwamba alikaa na watoto hao kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini wazazi wao hawakuwahi kulalamika kwamba walikuwa wakinyanyaswa kingono wakati huo.

“Niliwaweka watoto hao kwa muda wa kati ya miezi miwili na miezi mingine 9-10 na sikujua kwamba walikuwa wananajisiwa kwani wazazi wao hawakuwahi kuripoti chochote kuwa ninawachafua watoto au kugundua chochote kama hicho,” alisema.

Wakati akiwasilisha ushahidi wake, afisa wa uchunguzi Inspekta Mkuu Everlyne Mboya, alisema mshtakiwa alitumia mazingira magumu ya familia hizo kuwashawishi.

Hakimu Mkuu, Bi Ivy Wasike, alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kwa kiwango cha kuaminika madai yaliyotolewa dhidi ya mshtakiwa.

Hukumu inatarajiwa kutolewa Oktoba 14 mwaka huu.

Kulingana naye, mshtakiwa aliwafanya wazazi wa watoto hao kumwamini kuwa hana nia mbaya kiasi cha kumruhusu kukaa na watoto wao na hata kusafiri naye hadi bara kwake kijijini Nyeri ambapo alizidi kutenda unyama huo.

Mshtakiwa alipewa siku 14 kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama huku hukumu yake ikitarajiwa kutolewa Oktoba 14.