Hoja ya kunitimua ni kinyume na sheria, na imesheheni uongo, Gachagua aambia mahakama
KATIKA juhudi za mwisho mwisho za kujinusuru dhidi ya kumtimua mamlakani, Naibu Rais Rigathi Gachagua ameomba mahakama kuzuia Bunge kujadili hoja ya kumfuta kazi akisema imo kinyume na sheria na imejaa uongo.
Katika kesi aliyowasilisha kortini Alhamisi adhuhuri, Bw Gachagua pia anataka mahakama isimamishe mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa umma mpaka pale mipango ya ukusanyaji maoni itawekwa sawa kulingana na sheria.
Anadai kwamba hoja ya kumtimua iliyowasilishwa Bungeni Jumanne inakandamiza haki zake na kwamba yeye ni mwathiriwa wa usulubisho wa kisiasa.
“Mpango wa kunitimua ni njama ya kubatilisha uamuzi wa wengi wa Wakenya ambao walinipigia kura kama Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” anasema Bw Gachagua.
Anazidi kusema kwamba hoja hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse ni ya “msingi hafifu ambao haufikishi vigezo vya kisheria ambavyo vinahitajika katika kung’oa mamlakani kiongozi.”
Anasema kutimua kiongozi mamlakani ni jambo la uzito mkubwa ambalo linahitaji kufanywa kwa kufuata Katiba na mchakato mzima unaohitajika.
Huku akitaka zoezi la kukusanya maoni ya wananchi lisimamishwe, Bw Gachagua anasema kwamba kwa jinsi lilivyopangwa sasa hivi, ni watu wachache tu watakaoshiriki.
“Vikao vya kukusanya maoni vimepangwa kufanywa katika eneo moja katika kila kaunti, na kwa sababu ya gharama ya usafiri na umbali mrefu, inamaanisha kwamba wengi wa wananchi hawatafaulu kuhudhuria katika zoezi hili la umuhimu mkubwa kitaifa ambalo linaathiri haki za kiuchaguzi za Wakenya milioni 14.1 ambao walishiriki kwenye uchaguzi wa urais wa 2022 ambapo nilichaguliwa kama Naibu Rais kwa jumla ya kura 7,176,141,” kesi hiyo inasema.