Habari za Kitaifa

Sababu za UDA kujitenga na Mswada kuongeza muhula wa rais

Na DAN OGETTA October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha United Democratic Alliance kinachoongozwa na Rais William Ruto kimejitenga na Mswada wa Seneta wa Nandi Samson Cherargei unaopendekeza muhula wa rais na viongozi wengine waliochaguliwa uongezwe kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Chama hicho tawala, tayari kinakabiliwa na mgawanyiko miongoni mwa maafisa wake wakuu kuhusu uamuzi wa kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua na kinahofia kushutumiwa kwa kuhusishwa na pendekezo la kuongeza muhula wa rais na viongozi wengine waliochaguliwa kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Katika barua iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa UDA, Omar Hassan, chama hicho kilisema “kimefahamu kwa wasiwasi na masikitiko makubwa kwamba mmoja wa viongozi waliochaguliwa wa chama amewasilisha mswada wa sheria unaolenga kubadilisha muhula wa kikatiba uliowekwa kwa wanaoshikilia nafasi za kuchaguliwa.”

Waandalizi na wafadhili wa Mswada huo, Bw Hassan alisema, wamejishughulisha na ufisadi wa kisheria, na hawakuwazia na kutafakari vya kutosha kuhusu historia, msingi wa kitaasisi na hitaji la kuweka muhula wa viongozi kuhudumu.

“Kwa hivyo chama kinajitenga na Mswada huo wa kuchukiza. Mswada huo hauendani na sera na matarajio yetu. Majaribio haya ya kisiasa na dharau kwa maadili yetu ya kikatiba lazima yakomeshwe!”

Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2024, ambao kwa sasa unashirikishwa kwa umma, unalenga kuongeza muda wa viongozi wote waliochaguliwa kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka saba.

Mswada huo pia unalenga kuunda afisi ya Waziri Mkuu, ambaye atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa wanachama wa chama au muungano wa vyama Bungeni.