Habari

Hoja ya kumtimua Gavana Mutai yatua seneti

Na VITALIS KIMUTAI, BENSON MATHEKA October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SENETI imepokea rasmi uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Kericho wa kumtimua mamlakani Gavana Erick Mutai, licha ya maagizo ya mahakama yaliyositisha shughuli hiyo.

Dkt Mutai analaumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa Katiba, matumizi mabaya ya afisi, na utovu wa nidhamu katika hoja ya kumtimua iliyowasilishwa na MCA wa Wadi ya Sigowet, Bw Kiprotich Rogony.

Hata hivyo, gavana huyo alipata agizo kutoka kwa Mahakama Kuu kuzuia Seneti kupokea uamuzi huo kufuatia kura iliyopigwa na madiwani mnamo Oktoba 2, 2024, kumwondoa afisini.

Akizungumza Alhamisi Spika wa Seneti Amason Kingi alithibitisha kupokea stakabadhi kutoka kwa Bunge la Kaunti ya Kericho kuhusu pendekezo la kuondolewa kwa Gavana Mutai.

‘Nimepokea stakabadhi kutoka kwa Bunge la Kaunti ya Kericho kuhusu pendekezo la kuondolewa afisini kwa kutimuliwa kwa Dkt Erick Kipkoech Mutai, Gavana wa Kaunti ya Kericho,’ akasema.

Bw Kingi aliongeza kuwa kwa wakati ufaao atawasilisha ujumbe kwa Seneti kuhusiana na azimio hilo na kueleza hatua zinazofaa kuchukuliwa.

Spika aliwaonya maseneta dhidi ya kujadili suala hilo hadharani, akionya kuwa inaweza kuathiri matokeo ya uamuzi wa seneti.

‘Ningependa kuwaonya maseneta kuacha kutoa maoni yao hadharani kuhusu suala hili kwani kufanya hivyo ni ukiukaji wa kanuni nambari 99 ya Seneti,”Bw Kingi alisema.

Wakati huo huo, Jaji Joseph Sergon wa Mahakama Kuu ya Kericho aliagiza Dkt Mutai aendelee kutekeleza majukumu yake ya ugavana hadi kesi aliyowasilisha itaposikizwa na kuamuliwa.