Wakenya waongezewa siku kutoa maoni kuhusu hoja ya kumtimua Gachagua
BUNGE la Kitaifa limeongeza muda wa shughuli ya ushirikishwaji wa maoni ya umma katika hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa siku moja zaidi hadi Jumamosi, Oktoba 5, 2024.
Kwenye taarifa ya Ijumaa, Oktoba 4, 2024, Karani wa bunge hilo Samuel Njoroge alisema shughuli hiyo sasa itaendeshwa katika afisi 290 za maeneo bunge na afisi 47 za Wabunge Wawakilishi wa Kaunti.
Bw Njoroge alieleza kuwa agizo lake limechochewa na amri iliyotolewa na Mahakama Kuu kwamba Wakenya wapewa fursa ya kutoa maoni kwa hoja hiyo katika angalau ngazi ya maeneo bunge.
“Kufuatia amri ya Mahakama Kuu ya Kerugoya kwamba Bunge la Kitaifa liandae vikao vya umma kutoa maoni kwa hoja hii karibu na wananchi katika maeneo bunge kutoa nafasi kwa wabunge kushirikisha wananchi ipasavyo, naagiza shughuli hiyo iendeshwe katika afisi za wabunge hao Jumamosi Oktoba 5, 2024,” Bw Njoroge akasema.
Karani huyo alisema kuwa afisi hizo zitakuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi (8.00 am) hadi saa kumi na moja jioni (5.00pm) kuwezesha ushirikishaji wa umma kwa hoja hiyo maalum.
Shughuli hiyo iliendeshwa Ijumaa katika kaunti zote 47 nchini, ambapo wananchi walihitajika kufika katika kituo kimoja kujaza maelezo yao kwenye fomu maalum.
Katika uamuzi wake, Jaji wa Mahakama ya Kerugoya Richard Mwongo aliagiza kuwa shughuli ya kukusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu hoja hiyo inapasa “kufanywa angalau katika ngazi za maeneo bunge ambako wananchi wengi wanaweza kufika kwa urahisi.”
“Sharti bunge liandae shughuli kama hizo za ushirikishaji umma karibu na raia angalau katika ngazi ya eneo bunge kutoa nafasi kwa wapiga kura wa wabunge wanaohusika na mchakato huo kitaifa kuwashirikisha na kuwapa mwelekeo kama wawakilishi wao,” akasema katika uamuzi wake.
Jaji Mwongo alitoa agizo hilo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Jane Njeri Maina aliyodai shughuli ya ushirikishaji wa umma uliofanywa Ijumaa, Oktoba 4, 2024 haikuwa sawa.
Alisema notisi iliyotolewa kwa shughuli hiyo ilikuwa fupi zaidi kwani ilichapishwa magazeti mnamo Jumatano Oktoba 3, 2024, siku mbili tu kabla ya siku ya kuendeshwa vikao hivyo.