Habari za Kitaifa

Munyaka akataa kunyaka wadhifa alioteuliwa na Ruto: ‘Sitaingia serikali iliyojaa malumbano’

Na PIUS MAUNDU October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANDANI wa Rais William Ruto ameacha wengi vinywa wazi kwa kukatalia mbali uteuzi wa uenyekiti wa kituo cha kusimamia rasilmali za kijenetiki za mifugo, KAGRC.

Mbunge wa zamani wa Machakos Victor Munyaka ametaja malumbano yanayoendelea serikalini kati ya Rais na Naibu wake Rigathi Gachagua kuwa sababu zake za kususia ajira hiyo.

Kwenye taarifa aliyotuma Jumapili, Oktoba 6, 2024, Dkt Munyaka analaumu ongezeko la joto la kisiasa lililosababishwa na mkwaruzano katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Baada ya kufikiria sana, kushauriana kwa mapana na kuzingatia hali ya siasa nchini inayotishia ufanisi wa ajenda ya serikali kustawisha uchumi, nimeamua kufanya uamuzi wa kukataa kazi hiyo kwa heshima,” alisema kupitia taarifa iliyoonwa na Taifa Leo.

Kupitia mahojiano na Taifa Leo, Dkt Munyaka, ambaye aliteuliwa na Rais William Ruto awali kuwa Waziri Msaidizi wa Ardhi, alisema amesikitishwa na mgogoro kati ya Rais Ruto na Naibu wake Gachagua.

“Wanachofanya vinara hawa wa Kenya Kwanza ni cha kushangaza hasaa kwa sisi ambao tuko katika familia ya Kenya Kwanza. Rais na naibu wake wanafaa kuelewana na kuunganisha familia,” alisema.

Dkt Munyaka amekataa wadhifa huo katika kipindi ambacho tukio hilo linaonekana kuwa la kumfurahisha mbunge huyo wa awali aliyemkashifu rais kwa ‘kuwaweka katika baridi’ wanajamii wa Ukambani kwa uteuzi na miradi ya maendeleo.

“Nyinyi nyote mnajua nimepagazwa jina la ‘Kamotho wa Ukambani’ ukizingatia uaminifu wangu kwa Ruto. Nilimtambulisha kwa Mbunge Vincent Musyoka (Mwala), Bw Johnson Muthama na Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai na kupitia juhudi zetu, eneo la Ukambani lilimpa Ruto kura 250,000.

“Hizi ndizo kura ambazo zilimwezesha kushinda uchaguzi wa urais. Ninamuuliza rafiki yangu, Rais Ruto, kuacha kutelekeza eneo la Ukambani kwa heshima ya Munyaka, Kawaya, Mbai na Muthama ambao walifanya kazi bila kuchoka ili ashinde. Tumeona kuna mwenendo ambapo Wakamba ambao wana nyadhifa za hadhi wakianza kuzipoteza,” alisema katika mazishi ya dada yake Rose Mueni kijijini Muthwani, Kaunti ya Machakos majuma matatu yaliyopita.

Dkt Munyaka alirejelea aliyekuwa mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kibiashara Nchini – Kenya National Trading Corporation (KNTC) Pamela Mutua, aliyekuwa mkuu wa Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) Joseph Kimote, aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya Jumba la Kimataifa la Mikutano Nchini KICC Adelina Mwau, aliyekuwa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Ununuzi wa Bidhaa za Matibabu (KEMSA) Andrew Mulwa na aliyekuwa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Udhibiti wa Matumizi ya Dawa za Kulevya (NACADA) John Muteti akiwataja miongoni mwa wakazi wa Ukambani ambao walipoteza kazi majuzi.

Alipodinda kunyaka kazi aliyopewa na rais, Dkt Munyaka alimshukuru kwa kumfikiria akisema anamtakia heri rais anapoendelea kuongoza nchi.