Madhabahu ya Subukia yatafuta Sh25 milioni kukarabati kisima cha maji ‘matakatifu’
Tafsiri: CHARLES WASONGA
USIMAMIZI wa Madhabahu ya waumini wa Kanisa Katoliki, ‘The National Marian Shrine’ eneo la Subukia, Nakuru umeazimia kuchangisha Sh25 milioni kuimarisha vifaa vilivyoko karibu kitengo chake cha kisima cha maji ‘matakatifu’.
Mradi huo unaongozwa na shirika la Conventual Franciscan Friars, linalosimamia sehemu kama hizo takatifu ulimwenguni.
Mahala hapo pa kufanyiwa maombi maalum hutembelewa kila mwaka na waumini wa Kanisa Katoliki na watu wasio waumini wa kanisa hilo.
Haja ya kutekeleza wa mradi huo unaolenga kuboresha vifaa mbalimbali katika kisima hicho asilia ilianza kushika kasi Aprili mwaka huu baada ya miundo kuidhinishwa na Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB).
Wakati huu miundo hiyo inasubiri idhini kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nakuru kabla ya kazi yenyewe kuanza.
Madhabahu hayo huvutia mahujaji kutoka Kenya na maeneo mengine ulimwenguni kila mwaka.
Wikendi iliyopita, karibu mahujaji 50,000 kutoka Kenya, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, Malawi, Zambia, miongoni mwa nchini zingine walikongamana mahala hapo kwa maombi maalum.
Wengi wanaamini kuwa maji kutoka kisima hicho katika madhabahu ya “The National Marian Shrine” Subukia yanaweza kuleta baraka, uponyaji na mwamko mpya kiroho.
Mahujaji pia hufika hapo kutafuta mwelekeo kiroho, maombi na kutoa shukrani kutokana baraka walizozipata.
Hata hivyo, eneo la karibu na kisima katika madhabahu hayo limeshuhudia uharibifu kutokana na majanga ya kimaumbile na shughuli za binadamu.
Kwa hivyo, mradi huo unalenga kuimarisha muonekano wa eneo linalokaribiana na kisima hicho na kuboresha mandhari yake ili yafikie viwango vya kimataifa.
Wataalamu wa mipango wanasema hatua hiyo itahakikisha kuwa mahala hapo panafikia viwango vya madhabahu makuu ulimwenguni kama vile; “National Shrine of the Immaculate Conception”, “National Shrine of Mary, Mother of the Church” iliyoko Amerika na madhabahu ya “Basilica of Our Lady of Guadalupe” yaliyoko jijini Mexico City, nchini Mexico.
“Kando na kulihifadhi mahala hapa patakatifu tunalenga kupata faida ya kiroho, kukuza tamaduni na ushirikiano wa kijamii,” akasema Kasisi Vincent Opuba, Naibu Mkurugenzi wa ‘Subukia National Shrine’, alipotembelea mahala hapo Ijumaa kukagua hali yake.
Alisema kuwa ukarabati huo unaingiliana na kujitolea kwa Kanisa Katoliki utunzaji wa mazingira kulingana na ujumbe wa Papa Francis kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
“Sharti tutunze mazingira yetu kwa sababu maumbile huwa haisamehe binadamu. Sharti tufanye hivyo kwa kupanda miti ili kutunza vianzo vya maji,” Kasisi Opuba akaongeza.
Kamati tekelezi chini ya uenyekiti wa Jaji Alfred Mabeya imeundwa kukusanya fedha za kufadhili mradi huo.
Wanachama wengine ni; Sylvia Karuga (Naibu Mwenyekiti), Jerono Talam (Katibu), Linus Muigai (Naibu Katibu), na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Habari la Nation (NMG) Wilfred Kiboro ambaye ni mwanachama.
Wakati wa ukaguzi wa eneo hilo, Jaji Mabeya alisisitiza kuwa haja ya kuboreshwa kwa eneo hilo ili kukifanya kisima hicho kufikia ubora wa kimataifa.
“Jengo la sasa katika eneo hili linalokaribiana na kisima cha maji matakatifu halifai kwa mahala patakatifu lenye hadhi ya kitaifa. Hamna sehemu ya watu kukaa na madhabahu halisi yako katika hali mbaya. Tunataka mahujaji kufanya maombi katika mazingira matulivu na yasiyo na usumbufu wowote,” Jaji Mabeya akasema.
Hata hivyo, kamati hiyo inakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya mahitaji ya ujenzi na gharama ya usafirishaji hadi eneo hilo.
“Huu ni mradi wenye manufaa makubwa na ninawaomba Wakenya kuchangia ufanisi wake ili kufikia lengo la kuboreshwa madhabahu haya,” Jaji Mabeya akasema.
Ikikamilishwa, mradi huo utapiga jeki mji wa Subukia kiuchumi kwa kuvutia mahujaji zaidi.
Ili kutunza mazingira, kamati hiyo inapanga kuhakikisha kuwa miti inayotunza maji kama vile mianzi (bamboo) imepandwa kuzunguza chemichemi hiyo.
Mhandisi anayesimamia mradi huo Joseph Waweru Githung’a alieleza kuwa miundo mipya itatoa nafasi kwa watu kupitia na hivyo kuzuia uharibifu wa mazingira.
“Kibanda kitakachojengwa kitatumika na mahujaji huku muonekano asilia ukidumishwa na virembesho vichache vya kisasa vikiwekwa,” akasema.
Dk Kiboro alieleza umuhimu wa kiroho wa mahala hapo patakatifu akisema kuwa huvutia mahujaji kutoka sehemu mbalimbali nchini na ng’ambo.
“Nimetembelea sehemu mbalimbali takatifu ulimwenguni katika nchi za Ureno, Roma Italia na Israel ya zimejengwa kudumu kwa karne nyingi huku zikivutia watu wengi. Kwa hivyo, tunataka kuimarisha miundo msingi hapa ili kufikia viwango vya kimataifa ili mahujaji watapokuja, wapate mahala patulivu pa kufanyia maombi,” Dkt Kiboro aliambia Taifa Leo.
Alielezea kusikitishwa na hali ya miundo mbinu mahala hapo patakatifu akisema iko katika hali mbaya zaidi.
“Nasi hapa Afrika tunapaswa kuwa na sehemu maalum takatifu tunazoona sehemu mbalimbali ulimwenguni. Nimeshtuka na kushangaa. Miondo msingi na vifaa karibu na kisima iko katika hali mbaya zaidi. Huu ni wakati wetu kuleta mabadiliko kwa kujenga mahala patakatifu kuafiki Kenya na kufikia viwango vya kimataifa,” akasema.
Ukarabati wa kisima hicho tayari umeanza kuleta mazuri katika eneo hilo kwani mwekezaji mmoja anajenga hoteli kubwa zaidi karibu na madhabahu hayo.
Hii inaonyesha kuwa mahala hapo patakatifu pana uwezo wa kuwa kitovu wa ustawi wa kiuchumi eneo hilo kando na kuwa kitovu wa lishe la kiroho.