Habari

Gavana Dhadho Godhana, Mbunge Hiribae Said wanyakwa kufuatia vita vya kijamii Tana River

Na NYABOGA KIAGE, STEPHEN ODUOR October 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAELEZO yameibuka kuhusu jinsi Gavana wa Tana River Godhana Dhadho na Mbunge wa Galole Hiribae Said Buya walivyokamatwa kufuatia mapigano ya kijamii yanayoendelea katika kaunti hiyo.

Gavana Dhadho alikamatwa Jumamosi, Oktoba 12, asubuhi baada ya kufika katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) jijini Nairobi, huku mbunge huyo akikamatwa nyumbani kwake Nyali.

Mbunge huyo alipelekwa katika kituo cha polisi cha Makupa.

Mbunge huyo alikuwa wa kwanza kukamatwa, jambo lililomfanya gavana huyo kujisalimisha katika makao makuu ya DCI.

Kwa sasa gavana huyo anahojiwa katika makao makuu ya DCI kuhusu mapigano yanayoendelea Tana River.

Mkuu wa DCI Mohamed Ibrahim Amin alisema wawili hao walikamatwa kwa kushindwa kutii wito wa kufika kwa wapelelezi kuhojiwa kuhusiana na mapigano yanayoendelea ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 14.

“Ni kweli tulimkamata Gavana wa Tana River na Mbunge wa Galole. Wawili hao walikuwa wameitwa katika afisi zetu kuhusiana na mapigano hayo lakini walikataa kuheshimu wito huo,” alisema.

Bw Amin alisema uchunguzi kuhusu matukio yaliyosababisha mapigano hayo unaendelea na hatua zitachukuliwa kwa watakaopatikana na hatia.

Kukamatwa huko kunajiri saa 24 tu baada ya kaunti ndogo mbili katika Kaunti ya Tana River kutangazwa kutokuwa salama na hatari.

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, usalama umeimarishwa ndani ya Kaunti Ndogo za Bangale na Tana Kaskazini.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, katika notisi ya Gazeti la Serikali, alisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa kufuatia mashauriano mapana ndani ya sekta ya usalama.

“Katika kutekeleza mamlaka aliyopewa na kifungu cha 106 (1) cha Sheria ya Huduma ya Polisi ya Kitaifa, 2011, Waziri wa Masuala ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, kwa kushauriana na Baraza la Usalama la Kitaifa, anatangaza baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Tana River kuwa hatari kwa usalama,” alisema.

Maeneo mahususi ndani ya Kaunti Ndogo ya Bangale ni pamoja na Madogo, Areri, Saka, Sala, Mororo na Mbalambala.

Yale ambayo yataathiriwa ndani ya Kaunti Ndogo ya Tana Kaskazini ni pamoja na; Hirimani, Hosingo, Dukanotu, Chewele, Nanighi na Bura.

Wakati huo huo, Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) pia imetoa onyo kali kwa watu wanaomiliki silaha katika maeneo yaliyotajwa hapo juu.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema kwa kuwa eneo hilo limetangazwa  kuwa hatari, NPS inakataza umiliki wa silaha katika maeneo hayo.