Habari

Mwanamuziki Princess Jully maarufu kwa kibao ‘Dunia Mbaya’ aaga dunia

Na CHARLES WASONGA, FRIDAH OKACHI October 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWANAMUZIKI mashuhuri wa mtindo wa Benga Princess Jully amefariki.

Mwanamuziki huyo (jina halisi Juliana Auma) maarufu kwa kibao chake, “Dunia Mbaya” alifariki Jumamosi, Oktoba 12, 2024, katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Migori ambako amekuwa akipokea matibabu kwa kipindi cha miezi miwili.

Isipokuwa kibao “Dunia Mbaya” Princess Jully aliimbo nyimbo zake zingine kwa lugha yake asilia, dholuo.

Mmoja wa wanawe wa kiume Bradley Ogudah aliambia Taifa Dijitali kwamba mamake alipoteza ufahamu mwendo wa asubuhi kabla ya kukata roho mwendo wa saa nane za mchana.

“Amekufa. Amekuwa akiugua kwa miezi miwili,” akaeleza.

Princess Jully, 51, alipata umaarufu kati ya miaka ya 1990 na 2000 kutokana na kibao hicho “Dunia Mbaya” kinachosheheni maudhui ya kuonya watu dhidi ya kuambukizwa ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Marehemu ni mke wa tatu wa marehemu Jully Okumu (Prince Jully), mwanamuziki aliyechomoa vibao “Malo Malo” (Juu Juu) na “Akuru” (Njiwa), miongoni mwa vingine.

Prince Jully alikuwa mwanzilishi wa bendi ya Jolly Boys band, alikufa mnamo 1997.

Mwaka 2015, aliomba serikali imsaidie katika juhudi zake kuhamasisha Wakenya kuhusu Ukimwi.
“Wimbo wangu Dunia Mbaya ulipozinduliwa, kila mtu aliujua; hata maafisa wa serikali waliimba mashairi ya wimbo huo. Uliangazia hali ya wale wanaoishi na HIV. Serikali inapaswa angalau kunishughulikia na kutambua mchango wangu katika kupambana na janga la Ukimwi kupitia muziki wangu,” alisema Princess Jully.