Makala

Jinsi wimbo ‘Dunia Mbaya’ wa Princess Jully ulivyosaidia wengi kuogopa Ukimwi miaka ya tisini

Na AMOS NGAIRA October 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWIMBAJI maarufu Princess Jully (Lilian Auma Aoko) anaendelea kuombolezwa na kutajwa kama aliyeibua ufahamu mkubwa na kutoa onyo dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Princess Jully aliaga dunia Jumamosi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Migori ambako amekuwa akitibiwa baada ya kuugua kwa muda mrefu. Anafahamika sana kutokana na wimbo ‘Dunia Mbaya’ ambao ulivuma sana miaka ya 90 na 2000.

Mwanamuziki Johny Magneto ambaye aliuimba wimbo huo ulioachiliwa 1995 na Princess Jully, alimrejelea kama mwimbaji aliyekuwa na hekima ambapo nyimbo zake zilijikita kuhusu masuala yalikuwa yakiathiri jamii.

“Ni yeye alitunga mistari ambayo ilifanya wimbo huo upendwe na sio mashabiki tu bali hata wanachama wa bendi yake. Nyimbo zake nyingi zilikuwa na mafunzo na ujumbe kwa jamii,” akasema Magneto ambaye pia ni shemejiye Princess Jully.

Bw Magneto ambaye alikuwa nduguye Prince Jully (mumewe Princess Jully) alikuwa mchezaji mahiri wa gita kwenye bendi ya Maroon Commandoes Nairobi. Prince Jully aliaga dunia mnamo 1997.

Wanamuziki Emily Nyaimbo, Queen Babito na Atis Pesa pia walimwomboleza Princess Jully wakisema alichangia sana katika kuwashaajisha wazamie fani ya muziki.

Wanasiasa kadhaa nao walituma rambirambi zao huku Waziri wa Fedha John Mbadi akisikitikia mauti ya Princess Jully na kusema muziki wake ulisaidia eneo la Nyanza kuhamasishwa kuhusu virusi vya ukimwi.