Habari za Kitaifa

Jaji Mkuu ajibu maombi ya Gachagua kwa kuteua jopo la kusikiza kesi zake sita

Na SAM KIPLAGAT October 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JAJI Mkuu Martha Koome Jumatatu aliteua jopo la majaji watatu ili waamue kesi sita ambazo ziliwasilishwa kupinga mchakato wa kumwondoa mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bi Koome alimteua majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt Freda Mugambi kusikiza kesi hizo sita ikiwemo moja ambayo iliwasilishwa na Bw Gachagua mwenyewe.

Katika uamuzi wake Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu ilikubaliana na mawakili wa Bw Gachagua wakiongozwa na Paul Muite kuwa masuala sita ambayo yaliibuliwa, yaliyokuwa na uzito kwa kuwa yalikuwa ya kikatiba.

“Ikizingatiwa kuwa kesi hizo zinafuatiliwa sana na umma kwa sababu naibu rais wa nchi anaondolewa mamlakani, ni uamuzi wangu kuwe na jopo litakaloangazia mchakato uliofuatwa iwapo unawiana na katiba au la,” akaamua Jaji Mugambi.

Kati ya masuala ambayo yatazingatiwa ni kanuni za Bunge la Kitaifa ambazo zilitumiwa kumtimua Bw Gachagua. Naibu Rais alisema kuwa kanuni hizo ziliweka siku 12 pekee kukamilisha mchakato wa kumtimua, siku ambazo ni chache zaidi.

Bw Gachagua pia anadai kutolewa kwa siku hizo chache kulisababisha mikutano ya ushirikishaji wa umma kuharakishwa na raia kutoshirikishwa vilivyo jinsi katiba imeamrisha.

Bw Muite pia alisema Bunge la Kitaifa liliegemea upande moja katika mchakato huo wa kumtimua naibu rais.  Bunge lilijitetea likisema naibu rais alipewa muda wa saa mbili kujitetea mbele ya wabunge

Jaji alisema kuwa ni haki kwa raia kufahamu iwapo sheria za sasa zinawapa muda mwafaka wa kushiriki vyema mchakato wa kumwondoa Naibu Rais.

Mnamo Jumanne asubuhi, Jaji Chacha Mwita atatoa uamuzi iwapo mahakama itazuia Seneti kujadili na kuipigia kura hoja ya kumtimua Bw Gachagua ambayo ilipitishwa na Bunge la Kitaifa.