Njaa yanukia katika serikali za kaunti baada ya Seneti, Bunge kukosana kuhusu mgao
KAUNTI huenda zikakabiliwa zaidi na upungufu wa fedha baada ya Bunge la Kitaifa kukataa Mswada wa Marekebisho ya Mgao wa Fedha 2024 ambao ungetengea magatuzi yote 47, Sh400 bilioni.
Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa imedumisha pendekezo la kuzipa kaunti mgao wa Sh380 bilioni kwa mujibu wa Mswada wa Mgao wa Fedha 2024.
Kutokana na tofauti kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa, sasa kutabuniwa kamati ya upatanishi kati ya mabunge hayo mawili kupata muafaka kuhusu mswada huo.
“Kamati hii imekataa marekebisho yaliyofanywa na kuongeza mgao kwa kaunti hadi Sh400 bilioni,” kamati hiyo ikasema kupitia ripoti iliyowasilishwa bungeni.
Bunge la Kitaifa lilikuwa limependekeza mgao ambao ulikuwa uelekee kwa kaunti ubaki Sh380 bilioni huku ikisema kuwa kwa sasa serikali inakabiliwa na uchechefu wa kifedha.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi sasa watalazimika kubuni kamati ya pamoja ili kuibuka na mswada ambao unakubaliwa na mabunge yote.
Kwa mujibu wa katiba iwapo kamati hiyo haitakubaliana ndani ya siku 30, basi mswada huo utakuwa umeporomoka. Wiki mbili zilizopita Seneti ilibatilisha Sh380 bilioni kwa kaunti na kusema hawatakubali chini ya mgao wa Sh400.1 bilioni ambayo iliidhinishwa chini ya Sheria ya Ugavi wa Mapato kwa Kaunti 2024 (DoRA).
Sheria hiyo iliangaziwa upya kupunguza mgao wa bajeti kufuatia kuanguka kwa Mswada wa Fedha 2024.
Rais William Ruto mnamo Juni alilazimika kuondoa Mswada wa Fedha 2024-25 kutokana na maandamano yaliyotanda nchini ambapo waandamanaji walivamia bunge wakilalamikia ushuru mwingi katika mswada huo.
“Nakataa kutia saini Mswada wa Fedha 2024 na kurejesha mswada huo kwa Bunge la Kitaifa kuondoa vifungu vyote,” akasema akiarifu bunge kuhusu suala hilo.
Serikali ilikuwa ikilenga kupitisha mswada huo ili kupata Sh347 bilioni mwaka wa fedha 2024/25 ndipo ijaze mwanya ambao ulikuwa katika bajeti yake ya Sh3.92 trilioni.
Maseneta wakipitisha mgao wa Sh400.1 bilioni, walikataa kupunguza Sh10 bilioni kwa kaunti kufuatia kutotiwa saini kwa Mswada wa Fedha 2024.
Seneta wa Mandera Ali Roba ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Bajeti alisema kuwa Bunge la Kitaifa lilikosea kwa sababu upungufu huo ulistahili kuhimiliwa na serikali kuu na ile ya kaunti.
Bw Roba alisema kuwa bajeti ilipunguzwa kutoka Sh3.9 trilioni hadi Sh2.6 trilioni na akapendekeza kuwa serikali ya kitaifa ipate Sh2.23 trilioni nazo kaunti zibakie na Sh400.16 bilioni jinsi ambavyo ilipitishwa kwenye Sheria ya Ugavi wa Mapato.