Michezo

SPRINT SKATING CLUB KENYA: Mwamko mpya katika mchezo wa kuteleza kwa viatu vya magurudumu

January 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

SPRINT Skating Club Kenya ni klabu ya mchezo wa kueteleza kwa viatu vya magurudumu yenye matawi yake katika kaunti 20 kati ya 47  nchini. Tayari imejizolea washiriki zaidi ya 150 na mashabiki wengi wasioweza kukadirika.

Umaarufu wake hauna kifani. Japo inaaminika mchezo wa huu ni wa mataifa ya bara ulaya, wachezaji humu nchini wameanza kuukumbatia na hata kuandaa mashindano ya kitaifa na kanda sawia ili kuonyesha ujuzi wao.

Wametengeneza katiba ya sheria za kuwaongoza katika shughuli zao za kila siku ili kuyapanga malengo .

Wakiwa gumzo mjini Nakuru wao huteleza kwa mikogo na kupenya baina ya magari wakiwa wamezingatia usalama.

Wachezaji wa Sprint Skating Club Kenya wakifanya mazoezi. Picha/ Richard Maosi

Waendeshaji bodaboda wamewapatia lakabu nyingi kama vile ‘malofa’ lakini hili halijawakatiza tamaa wakiamini hakuna kizuri kinachokosa dosari.

“Sisi ni vijana tuliojiwekea malengo maishani,tunachojaribu kufanya ni kufuata ndoto zetu  bila kujali kejeli za watu,” Wycliffe Onduso mmoja wa wachezaji alisisitiza.

Mchezo wenyewe humpasa mshiriki kutumia viatu vya magurudumu kwa stadi kuu ili aweze kutamba .Mbali na kusawazisha uzani wa mwili , asipoteze dira atafaa kutumia kasi akiwa makini.

Vyombo vya usalama kuanzia kichwani hadi kwenye mafundo ya mikono na miguu

Taifa Leo Dijitali ilipiga kambi katika makao yao rasmi Standard Chartered Grounds kaunti ya Nakuru ili kupata uhondo wa mchezo huu.

Vincent Muli mchezaji wa Sprint Scating Club Kenya akionyesha ujuzi wake kabla ya shindano. Picha/ Richard Maosi

Mkufunzi Vincent Muli anasema alianzisha kundi la wachezaji 30 mnamo 2015,kusudi lake kuwahamasisha watoto wanaozurura mitaani.

Amehitimu na shahada ya uhandisi kutoka chuo cha Egerton lakini kwa sababu ya ukosefu wa ajira aliamua kujiajiri na kuwaajiri vijana wenzake.

Aghalabu Sprint Skating Club Kenya hutumika na kampuni tajika kutoa matangazo ya kibiashara kwa malipo maalum.

Uwezo wa kusafari mwendo mrefu huku wakitumbuiza watazamaji ndio hunogesha shughuli.

Wanatumia mchezo huu kutangaza bidhaa pamoja na kuzisambaza.Pia serikali ya kaunti imekuwa ikiwatumia  kutumbuiza wageni katika tamasha za kitaifa kama vile siku ya Mashujaa uwanjani Afraha.

Baadhi ya wachezaji wa Sprint wakipumzika baada ya safari ndefu katika barabara ya Nakuru-Nairobi. Picha/ Richard Maosi

Mbali na hayo Muli alipania kuwapatia tajriba na ujuzi wa bure vijana wake, katika mchezo wenyewe ili waje kuwa watu wa kujitegemea katika jamii hasa katika jukwaa la michezo.

“Kama tujuavyo siku hizi kipaji kinalipa kama kazi nyingine,ilikuwa ni uamuzi wangu kutumia hii spoti kama chambo kunasa vijana,”alisema.

Kwa kuwa wengi wa washiriki hawakumudu gharama ya usajili alihakikisha wenye talanta ya kipekee wanapata nafasi ya kwanza kujiunga na kikosi .

Takriban siku zinavyosonga timu ya Sprint Skating Club Kenya imepata mashiko na kuigwa sio tu katika kaunti ya Nakuru, bali pia Afrika Mashariki.

Mchezaji Felisia Kimani akijizatiti kumaliza mkumbo wa mwisho akifanya mazoezi katika eneo la Lanet. Picha/ Richard Maosi

Majukumu yake mengi yakiwa ni pamoja na kuchangisha fedha kwa miradi ya kuinua jamii,Kutumia michezo kuhamasisha kuhusu uozo , majanga sugu kama vile mihadarati na kuwasaidia vijana kujiajiri kwa kutoa ushauri nasaha wa bure.

Wamekuwa wakipeperusha bendera ya taifa katika nyuga mbalimbali duniani na kujizolea medali na vyeti.

2017 walishiriki katika michuano ya African Championship kwa kumtuma  mwakilishi mmoja Cairo taifa la  Misri.

Japo Wizara ya Michezo haikuwagharamia walifanikiwa kupata tiketi ya pasipoti kwa mwenzao Vincent Muli aliyeibuka nambari saba katika michuano hiyo, kati ya Octoba 28 hadi Novemba 3, 2017.

Mnano 2016 waliibuka kidedea nchini kupitia nyota Felisia Kimani aliyetamba mita 100  Mombasa.

Kikosi chao kilionyesha ubabe Octoba 2016 walipoibuka nambari mbili katika jumuia ya michezo iliyoandaliwa Kisumu na kuleta timu 12 kutoka Afrika Mashariki na kati .

Felisia Kimani anasema licha ya kuwa mwanafunzi chuoni Rift Valley Technical  Institute Nakuru, anatumia wakati wake vyema kuhakikisha anahudhuria darasa na kufanya mazoezi.

Kijana akionyesha ujuzi wake katika mchezo wa kuteleza kwa magurudumu mjini Nakuru wakati wa mazoezi. Picha/Richard Maosi

Anatoa shukran za dhati kwa wazazi wake waliomtambua mapema na kumhimiza azingatie kipaji na masomo.

“Mchezo unanipatia tulizo la mawazo baada ya siku nzima darasani,” alisema.

Hata hivyo gharama kubwa wanayokumbana nayo ni kununua viatu vya magurudumu na jezi za kushiriki mazoezi ambazo ni ghali mno.

Kenya Federation of Rollers (KFR) ni mwavuli unaowaleta pamoja wachezaji wanaoteleza kwa viatu vya magurudumu Kenya.

Wamekuwa wakiratibu mashindano ya ligi nchini,mbali na kuwaandalia hafla za kushindana japo mara moja moja.

Hivi sasa wanajifua kushiriki katika mapambano ya Olimpiki Japan 2020 wakiamini mechi za kujipima zitakuwa muhimu kuwastawisha.