Sherehe ya kufurahia shoo ya Glen Washington yakatizwa kwa kupigwa risasi na afisa mlevi wa polisi
JIMMY Ngugi alipoamua kutembelea klabu moja ya usiku mjini Naivasha ili kuhudhuria shoo ya nyota wa reggae kutoka Jamaica Glen Washington mnamo Oktoba 13, 2024, alikuwa mwenye furaha sana.
Akiwa na marafiki zake walifika ukumbini tayari kujiburudisha na kuufurahia usiku huo. Hakujua kuwa usiku ungegeuka kuwa mbaya kwake. Bw Ngugi, 30, alikuwa ameegesha pikipiki yake nje ya klabu alipomuona mwanamume aliyeonekana kuwa mlevi akiikojolea.
Alimkabili mtu huyo na wakagombana kwa muda mfupi kabla ya mtu huyo kuchomoa bunduki na kumpiga risasi.
Tukio hilo lilitokea nje ya kilabu, likawashtua watazamaji na waliokuwa kwenye shoo. Baadaye iliibuka kuwa Ngugi alikuwa amepigwa risasi na afisa wa polisi aliyejihami kwa bastola. Kulingana na walioshuhudia, makabiliano hayo yalianza pale afisa huyo wa polisi aliyevalia nguo za kiria, aliyeripotiwa kuwa mlevi, alipokojolea pikipiki ya Ngugi, iliyokuwa imeegeshwa nje ya klabu hiyo maarufu ya usiku.
Ngugi alikabiliana na afisa huyo kuhusu hatua yake, na kusababisha ugomvi mkali. Mmoja wa marafiki waliokuwa wameandamana na Ngugi, aliambia Taifa Leo kwamba afisa wa polisi ambaye alionekana kuwa amelewa alichomoa bastola yake na kumpiga mwathiriwa risasi shingoni, kabla ya kuondoka eneo la tukio.
“Nilimwona afisa huyo akikojolea pikipiki, kabla ya mabishano kutokea. Wakati wa ugomvi huo, afisa huyo alichomoa bastola yake na kumpiga risasi Ngugi. Risasi hiyo ilipita kwenye shingo ya Ngugi, na kumpasua mfupa wa shingo,” alisema rafiki huyo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu ya uzito wa suala hilo.
“Rafiki yangu Ngugi alianguka chini akiguna kwa maumivu na kujaa damu. Tulimkimbiza katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha, ambako anaendelea na matibabu,” akaongeza rafiki huyo ambaye alishuhudia ufyatuliaji huo.
Ilibainika kuwa Ngugi alipigwa risasi na afisa wa Kitengo cha Polisi cha Miundombinu muhimu (CIPU).
Muuguzi katika hospitali ndogo ya kaunti ya Naivasha alifichua kuwa Ngugi bado anaendelea na matibabu, lakini yuko katika hali mbaya.
Akizungumza kutoka kwa kitanda cha hospitali alikumbuka matukio kabla ya kupigwa risasi akisema; “Nilitaka kujua kwa nini aliamua kukojolea pikipiki yangu, badala ya kwenda chooni, lakini alinipiga risasi shingoni. Kwa bahati nzuri nilikimbizwa hospitalini huku nikivuja damu, na matabibu walifanikiwa kuokoa maisha yangu,” Ngugi alisema wakati wa mahojiano.
“Ninamuomba Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai kuhakikisha afisa huyo wa polisi anakamatwa na kufikishwa mahakamani,” aliongeza Ngugi.