Habari za Kitaifa

Kikao cha seneti chaahirishwa baada ya Gachagua kugonjeka ghafla

Na CHARLES WASONGA October 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesemekana kuugua ghafla na anapokea matibabu hospitalini, hivyo amefeli kujitokeza kujitetea mbele ya Seneti Alhamisi alasiri, Oktoba 17, 2024.

Kiongozi wa jopo la mawakili wake, Paul Muite, ameiambia Seneti kwamba mteja wake alifeli kufika kwa sababu amekimbizwa hospitalini kwa matibabu baada ya kuugua.

“Ninaanza kwa kuomba radhi kwamba naibu rais hayuko. Ningependa kuiambia Seneti kwamba Naibu Rais anaugua na yuko hospitalini kwa matitabu,” Bw Muite akasema.

Bw Muite aliomba apewe muda hadi saa kumi na moja jioni, ili amwasilishwe Bw Gachagua.

Wakili huyo mkuu alisema hayo baada ya Spika wa Seneti Amason Kingi kumwambia kuwa muda uliotengewa Bw Gachagua ulikuwa ukiyoyoma.

Baada ya Bw Kingi kushauriana na Kiongozi wa Wengi Aaron Cheruiyot na Kiongozi wa Wachache Stewart Madzayo, aliamua kusitisha kikao kwa muda hadi saa kumi na moja jioni.

“Baada ya wakili wa Naibu Rais kusema kuwa anaugua na baada ya kufanya mashauriano, naamuru kuwa kikao hiki kisimamishwe hadi saa kumi na moja jioni,” akasema Spika wa Bunge la Seneti.

Bw Kingi alisema hayo baada ya Wakili Muite kuahidi kuelekea hospitalini kukagua hali ya Bw Gachagua kisha kutoa ripoti kwa Seneti.

Hata hivyo, wakili huyo mwenye tajiriba ya muda mrefu hakufichua aina ya maradhi yanayosibu Bw Gachagua wala hospitali ambako alikimbizwa kwa matibabu.