Makala

Mahakama yaambiwa mwanariadha Tirop alikuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa

Na TITUS OMINDE, WINNIE ONYANDO October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAREHEMU mwanariadha mashuhuri Agnes Tirop, alikuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa kabla ya mauaji yake ya kikatili Oktoba 2021, shahidi katika kesi ya mauaji yake aliambia Mahakama Kuu mjini Eldoret.

Joseph Cheromei, kocha wa muda mrefu wa marehemu, alimweleza Jaji Robert Wananda kwamba alifahamishwa kuhusu uhusiano huo na meneja wa riadha wa Italia Giani Demadona.

Bw Cheromei alisema meneja huyo alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa marehemu baada ya kumweleza kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume aliyejulikana tu kama Bw Sawe.

Alisema kuwa mnamo Juni 2021, meneja huyo wa Italia alimuomba ampeleke Bi Tirop kwenye kambi ya mazoezi kabla ya mbio mbili kuu ambazo angeshiriki huko Tokyo, Japan, na Valencia, Uhispania.

“Niliagizwa nimpeleke Agnes kambini baada ya kujua kwamba alikuwa akipitia changamoto mikononi mwa Abraham Rotich ambaye alikuwa mumewe,” alisimulia Cheromei.

Bw Cheromei alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji ya Bi Tirop ambapo Rotich, mshukiwa mkuu wa mauaji yake, anakabiliwa na shtaka la mauaji.

Mshukiwa huyo anasemekana kumuua Bi Tirop mnamo Oktoba 13, 2021, katika nyumba yao ya mashambani iliyo karibu na mji wa Iten katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Rotich, ambaye yuko nje kwa dhamana ya Sh400,000, amekana shtaka la mauaji.

Anawakilishwa na wakili Ngigi Mbugua huku familia ya mwanariadha aliyeuawa ikiwakilishwa na Richard Warigi.

Marehemu huyo aliuawa siku chache tu baada ya kuwasili nchini kutoka mbio za kimataifa katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo ambapo alimaliza wa tano katika mbio za mita 5000.

Shahidi mwingine, Miriam Rotich, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi, aliambia mahakama jinsi mshukiwa mkuu, shemeji yake, alivyomwomba ampe gari lake ili kufanya shughuli zake katika mji wa Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

“Nilimpa gari langu baada ya kushauriana na mume wangu Cornelius Rotich,” aliongeza.

Alisema siku ambayo alimpa Rotich gari lake, alionekana mwenye asiwasi na kutokwa na jasho jingi.