Makala

Chifu Misheveve: Mzungumzaji hodari, video yake ya 2010 imemgeuza staa mitandaoni

Na JURGEN NAMBEKA October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA dunia ya sasa ambayo mtandao wa kijamii unaweza kufufua mambo yaliyosahaulika, mahojiano ya chifu mmoja kutoka Trans Nzoia, yaliyorekodiwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, yamesambazwa na kumfanya kiongozi huyo wa eneo dogo kuwa staa mtandaoni.

Chifu wa eneo la Saboti, Bw Protus Wechuli ambaye kwa sasa anafahamika kwa jina la utani “misheveve” ameinasa mioyo ya Wakenya mtandaoni na ucheshi wake wa kuelezea jinsi mzozo ulichukua maisha ya mzee mmoja kijijini kwao.

Chifu Wechuli amehudumu kwa miaka 16 sasa kwani alianza kazi hiyo mnamo 2007.

Alikuwa akieleza jinsi ambavyo mwanamume mmoja aliuawa na mwanawe kwasababu ya mzozo wa kifamilia. Mzozo huo ulitokana na mboga hiyo maarufu kutoka Magharibi mwa Kenya, iliyokuwa imepikwa na mamake, licha ya kijana huyo kutaka mboga mbadala. Mboga hiyo ya misheveve ni majani ya malenge ambayo huandaliwa na kuliwa kwa ugali.

Huku akiwa amevalia sare kamili zinazovaliwa na machifu, Bw Wechuli amefahamika kwa mazungumzo yake yaliyojaa ucheshi, mbwembwe na lafudhi ya kipekee ambayo huenda ikawafanya wasimuliaji kushikwa na wivu.

Video hiyo iliyofanywa na runinga ya televisheni ya QTV kueleza tukio hilo, ilichipuka katika mitandao mbalimbali, vijana wakitumia sauti hiyo kutengeneza video za ucheshi licha ya uzito wa lililokuwa likizungumziwa.

“Tulinyata nyata na kufika pale katika tukio. Huyo kijana alitoka wakati wa magharibi. Akauliza mama, leo umepika mboga gani, mama akasema leo nimepika misheveve. Kijana alitaka ‘Salad’ na akagadhabishwa na kumsukuma mamake kutoka kwenye kiti moto. Babake aliingilia kati na kijana akamgonga babake akazimia. Alichukua hatua ya kinyasa na kutafuna vidole vya mzee kama omena,” akasema chifu huyo wa tano wa eneo hilo katika mahojiano.

Wakenya walikuwa wamempa sifa ya ucheshi Bw Wechuli akieleza kuwa hulka hiyo ilikuwa imemwezesha kutekeleza kazi yake inavyofaa.

“Ninafahamu kuwa kazi yetu kama machifu ni ya kupangua mabaya na kupanga mazuri. Na hauwezi kufanya hivyo ukiwa mgumu, lazima ujue njia ya kufikia wakazi. Na hiyo imenisaidia kutekeleza kazi,” akasema Bw Wechuli.

Video hiyo ya misheveve siyo video ya pekee inayoonyesha ucheshi wa chifu huyo, kwani Wakenya mitandaoni wamechapisha video zingine ambazo zinaashiria chifu huyo akitekeleza kazi yake kwa mbwembwe na furaha.

Video ya hivi punde zaidi ikiwa katika hafla ya serikali ya kaunti ya Trans Nzoia ambapo Bw Wechuli anamkaribisha waziri wa Kilimo wa kaunti hiyo Bi Phanice Khatundi.

“Bila kujikuna unywele wala utosi, namkaribisha waziri wa Kilimo. Je, mnaona yeye huoga kwa soda ya Fanta au vipi,” akasema katika video hiyo iliyomiminia sifa uwezo wake.

Aidha, Bw Wechuli, ambaye ana mke mmoja na watoto saba, ametumia uwezo wake kusuluhisha mizozo ya kijamii, akimmiminia sifa mkewe akisema yeye ndiye alimwezesha kufuzu kufanya kazi hiyo.

Isitoshe, anathamini sana masuala ya elimu akieleza kuwa kukosa elimu ni mwanzo wa kupoteza yote.

“Elimu ni kujua mengi kuhusu madogo na madogo kuhusu mengi. Ukosefu wa elimu ni hatari, kwani unaweza kumfanya mtu kupoteza kila kitu,” anasema chifu huyo.

Aidha, chifu huyo amewafanya Wakenya mtandaoni wasiotoka katika eneo la Magharibi kutaka kufahamu mengi kuhusu mboga hiyo ya misheveve, ambayo huandaliwa na wakati mwingine kutiwa maziwa.

“Huyu chifu ni mwerevu sana, anafahamu mengi, mzungumzaji mzuri, mzuri na watu na mwenye furaha sana,” akasema Bi Winfred Jemutai.