Divai ya matikitimaji
AGHALABU, divai nyingi zinazojulikana huundwa kwa matunda ya zabibu au beri.
Hata hivyo, ulijua matikitimaji (watermelon) yanatumika kutengeneza divai?
Matikitimaji ni matunda yanayoshabikiwa na wengi kutokana na virutubisho vyake kiafya.
Endapo hukujua, yanaunda mvinyo ambao hata wewe utaufurahia na kuupenda.
Katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Kibiashara Nairobi 2024, yanayoandaliwa kila mwaka na Chama cha Kilimo cha Kenya (ASK), Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kwenye mojawapo ya standi zake kilivutia waliohudhuria kufuatia mseto wa vinywaji.
Divai ya matikitimaji iliteka wengi, George Mathenge mtaalamu wa Masuala ya Sayansi ya Chakula akisema JKUAT iliingilia uundaji wa mvinyo huo kuokoa wakulima wanaopoteza mazao msimu wa mavuno.
Kwenye maonyesho hayo ambayo yalikuwa Makala ya 123 ya ASK yaliyofanyika kati ya Septemba 23 na 29, chuo hicho pia kilikuwa na divai ya mkaktusi (cactus).
JKUAT ni chuo cha kiserikali kinachotambulika kwa mafunzo na utafiti wa masuala ya kilimo na teknolojia.
Taasisi hiyo ilianza uchakataji wa divai ya matikitimaji 2006, na mwaka mmoja baadaye, 2007, bidhaa hiyo ikaingia sokoni baada ya kupewa idhini na Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS).
“Mbali na mashamba, ukizuru masoko mengi nchini (yale ya mazao mabichi), hutakosa kuona matunda yaliyotupwa na kutapakaa, matikitimaji yakiwemo. Ni jambo linaloatua moyo sana,” Mathenge anasema.
Mtaalamu huyu anaamini kwamba wakulima wanaweza kuhamasishwa jinsi ya kuongeza matunda thamani kwa kuyasindika (processing).
“Tikitimaji ni tunda lenye maisha mafupi, na mkulima au mfanyabiashara akikosa miundomsingi bora kulihifadhi litaharibika. Hata hivyo, ukiliongeza thamani kwa kuunda divai, bidhaa hii itadumu muda mrefu na kuteka bei bora,” anaelezea.
Bidhaa za pombe hudumu miaka na mikaka, kabla ufuniko wa hifadhi kufunguliwa.
Isitoshe, divai ya matikitimaji inateka soko bora Mathenge akidokeza kwamba kipimo cha mililita 750 chenye asilimia 12 ya kiwango cha pombe kinauzwa Sh1, 000.
Kwa sasa, JKUAT inaendelea kutafiti utengenezaji wa divai ya mkaktusi akiashiria kuwa mvinyo huo pia ukikaguliwa na kuidhinishwa na KEBS bei yake itakuwa sawa na ya matikitimaji.
“Mkaktusi umesheheni virutubisho vya Zinc; madini faafu na muhimu sana mwilini, hasa katika kuboresha afya ya wanaume,” Mathenge akaambia Akilimali wakati wa mahojiano katika Maonyesho ya ASK Nairobi, Jamhuri Grounds.
Kauli mbiu ya hafla hiyo ilikuwa ‘Uhamasishaji wa Kilimo Safi Kinachozingatia Hali ya Hewa na Mikakati Endelevu Kuboresha Ukuaji wa Uchumi’.
Wakulima wanaendelea kuwa mateka wa mabroka na bei yao mbovu, na uongezaji thamani mazao ya shambani kama vile kuunda divai ya matikitimaji ni hatua inayoweza kuwaokoa.
JKUAT hutoa mafunzo, japo kwa ada kwa watu binafsi na pia kupitia makundi.
Kulingana na Mathenge, kilo 200 za matunda ya matikitimaji zinatoa lita 80 ya juisi inayogeuzwa kuwa divai kupitia taratibu na fomula ya uundaji mvinyo.
Kiwango hicho kinazalisha lita 70 ya divai.
Wizara ya Kilimo inakadiria taifa hupoteza kati ya asilimia 20 hadi ya 30 ya mazao mabichi shambani, kwa sababu ya matatizo ambayo wakulima hupitia wakati wa mavuno.
Ukumbatiaji teknolojia za kisasa na bunifu, ni mifumo inayotajwa kuwa itasaidia kuokoa wakulima na wafanyabiashara dhidi ya kupoteza bidhaa.
Mbali na JKUAT, Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Nchini (KIRDI) pia hutoa mafunzo ya uchakataji.