Akili MaliMakala

Nyasi ya Juncao inavyookoa mwanahabari wa zamani kuendeleza ufugaji

Na SAMMY WAWERU October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SAMMY Kariuki alipofanya maamuzi kuweka chini mikrofoni, ukulima ulikuwa mojawapo ya shughuli za kibiashara alizopania kuingilia. 

Mwanahabari huyu wa zamani wa masuala ya kisiasa, alihudumu katika tasnia kwa zaidi ya miaka 20.

Miongo miwili ya kuwafahamisha mashabiki wake yanayojiri nchini na katika nyanja za kimataifa, aliamua kuingilia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

“Nina mapenzi ya dhati kwa ng’ombe wa maziwa, na nilichagua mkondo huo,” anasema.

Kariuki pia ni mfugaji wa kuku na kondoo.

Awali, maziwa aliyozalisha kwa kiwango kikubwa yalitumika kwa familia yake.

Sammy Kariuki, mwanahabari wa zamani ambaye amegeuka kuwa mfugaji wa ng’ombe wa maziwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Miaka kadha iliyopita, alikata kauli kugeuza ufugaji kuwa biashara kujiendeleza kimaisha.

Hata hivyo, gharama ya juu ya chakula cha madukani cha mifugo ilikuwa kikwazo kuunda faida.

Kuongeza chumvi au shubiri kwenye kidonda kinachouguza, Kariuki anasema aliandamwa na kero ya chakula duni – ambacho hakijaafikia ubora wa bidhaa.

Kwa kiasi kikubwa, alitegemea nyasi za mabingobingo (Napier grass), nyasi za kawaida na majani ya mahindi kulisha ng’ombe wake.

“Kiwango cha juu cha maziwa ambacho ng’ombe mmoja angetoa kwa siku kilikuwa lita tano,” anadokeza.

Ni kupitia programu kwenye runinga kuhusu mbinu za kushusha gharama ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, Kariuki alifunguka macho kuhusu nyasi mpya maalum nchini ambayo imegeuza ufugajibiashara wake kuwa wa kutabasamu.

Sammy Kariuki akikatakatia ng’ombe wake nyasi ya Juncao eneo la Nakuru. PICHA|SAMMY WAWERU

“Juncao, ni nyasi ya kisasa na iliyoboreshwa na ambayo imenisaidia pakubwa kushusha gharama ya ufugaji,” anakiri.

Anasimulia kwamba baada ya makala hayo ya runinga yaliyompevusha, alifanya utafiti na kugundua kwamba nyasi hiyo imesheheni virutubisho na madini faafu kwa mifugo, hasa wa ng’ombe wa maziwa.

Nyasi ya Juncao ilivumbuliwa na Mwanasayansi wa China, na imekuwa ikitumika nchini humo kwa muda wa miaka kadhaa.

Kichina, Jun inamaanisha Uyoga na Cao Nyasi.

Kando na kukuzwa kama malisho ya mifugo, nyasi hii ya aina yake inatumika kama kipandio chenye rutuba kuzalisha uyoga unaoliwa na binadamu. Upekuzi wa Akilimali kwenye tovuti ya http://www.juncao.org unaonyesha nyasi hii ndefu ya kijani kilichoshika, ilivumbuliwa 1980s na Prof Lin Zhanxi, ambaye alikuwa Mhadhiri wa Fujian Agriculture and Forestry University (FAFU), China.

Isitoshe, mtandao huo unaarifu teknolojia ya Juncao inaangazia usalama wa chakula kwa kuboresha mimea na mifugo, hivyo basi kuwa nguzo kuu dhidi ya kupambana na umaskini, kubuni nafasi za ajira na kuboresha mazingira.

Nyasi ya Juncao tayari imetua Barani Africa, haswa nchini Kenya.

Mfugaji Sammy Kariuki akielezea kuhusu kilimo cha Juncao shambani mwake Nakuru. PICHA|SAMMY WAWERU

“Nilianza kutumia Juncao 2022 na nimeona mabadiliko makubwa kwenye biashara yangu ya ufugaji,” Kariuki akasema wakati wa mahojiano kwenye shamba lake eneo la Lengenet, Rongai, Kaunti ya Nakuru.

Unapozuru boma lake, utakaribishwa na nyasi hiyo kwenye ua.

Akiwa na ng’ombe saba wa maziwa, mfugaji huyu ametenga ekari moja kulima Juncao.

Majuzi, anadokeza kwamba aliongeza ekari moja zaidi kwa minajili ya kilimo cha nyasi hii maalum.

Miaka miwili baada ya kuikumbatia, anakiri kiwango cha maziwa kimeongezeka mara dufu.

“Kwa sasa, ng’ombe mmoja anazalisha kati ya lita 12 hadi 15 kila siku,” anafichua, akikadiria kupunguza gharama ya ufugaji kwa karibu asilimia 60.

Kariuki hutoa mbegu za upanzi kutoka kwa Juncao Grass Technology Kenya, shamba la uzalishaji wa nyasi hii lililoko Nakuru, eneo la Kampi ya Moto.

Shamba hilo la ekari 50 lilianza kilimo cha Juncao nchini 2021, na lina matawi mengine Lodwar, Garissa, na Makueni.

“Nyasi hii ni rahisi kupanda na ina mazao mengi, na kiwango chake cha Protini kinakadiriwa kuwa asilimia 18.6,” anaeleza Edwin Wekesa, Meneja wa Mikakati Juncao Grass Technology Kenya.

Mbali na kutumika kulisha ng’ombe na kukuza uyoga, Wekesa anasema Juncao pia huchakatwa kuwa chakula cha samaki, kuku, mbuzi na kondoo.

Nyasi ya Juncao, kulingana na Edwin Wekesa pia inatumika kuunda silage. PICHA|SAMMY WAWERU

Vilevile, huunda silage.

Asili yake ikiwa China, Juncao ilivumbuliwa kama mojawapo ya mbinu kukabiliana na athari za tabianchi; ukame, na pia kuzuia mmomonyoko wa udongo, hivyo basi ni miongoni mwa teknolojia za kisasa kudhibiti athari hasi.

Inastahimili maeneo yanayopokea kiwango cha chini cha mvua.

Kenya inaendelea kukabiliwa na changamoto ya chakula cha mifugo, ikilazimika kuagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 80 ya malighafi.

Hali hii ilichochewa kuwa mbaya 2020, janga la Covid-19 lilipotua, ikiwa ni pamoja na nyongeza ya ushuru na ada za juu zinazotozwa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Hivyo, Juncao ni miongoni mwa malisho ambayo wakulima wanaweza kukumbatia ili kushusha gharama ya ufugaji.