Akili MaliMakala

Nyasi ya Juncao inavyolimwa

Na SAMMY WAWERU  October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NYASI maalum aina ya Juncao, yenye asilia ya China, inahimili mikumbo ya athari za tabianchi. 

Inanawiri sehemu zinazopokea kiwango cha chini cha mvua, na kiangazi au ukame si hoja vile kutokana na maumbile yake.

Ikiwa na sifa kemkem hususan kuokoa wakulima wanaoendeleza ufugaji, nyasi hii hurefuka hadi mita saba japo inakadiriwa kuwa na wastani kawaida wa mita nne hadi tano na kipenyo (diameter) cha sentimita moja na nusu (1.5) hadi mbili na nusu (2.5) cha tawi.

Edwin Wekesa, Meneja wa Mikakati Juncao Grass Technology Kenya akielezea jinsi nyasi hiyo hulimwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Chini ya taratibu na matunzo faafu kitaalamu, Edwin Wekesa, Meneja wa Mikakati Juncao Grass Technology Kenya, kampuni inayohamasisha ukuzaji wake nchini, anasema inakomaa kwa muda wa miezi mitatu pekee.

Mbegu zake ni matawi (cuttings).

Upanzi

Sammy Kariuki, mkulima aliyekumbatia nyasi hii kupunguza gharama ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, anasema huandaa mashimo yenye kina cha sentimita kumi (10) na kati ya mashimo mita moja na nusu (1.5) hadi mbili (2).

Kati ya laini ya mashimo, huipa nafasi ya mita moja na nusu (1.5) hadi mita mbili (2).

Meneja wa Mikakati Juncao Grass Technology Kenya, Edwin Wekesa akifafanua kuhusu upanzi wa Juncao. PICHA|SAMMY WAWERU

“Tawi bora zaidi ni lenye nodi (nodes) mbili (2), na zinapaswa kutazamishwa juu kisha zifunikwe kwa udongo kiasi,” Kariuki anaarifu.

Aidha, mkulima huyu hutumia mbolea ya mifugo kupanda Juncao, na anasema tangu akumbatie nyasi hii ya kipekee hajawahi kushuhudia kero ya wadudu na magonjwa.

Anasema hutegemea mvua kuilima.

Edwin Wekesa anadokeza kwamba ekari moja ina uwezo kuzalisha tani metri 180 kwa mwaka.

Juncao Grass Technology Kenya inahudumia zaidi ya wafugaji 1, 000 kote nchini.

Juncao Grass pia husagwa kuunda silage. PICHA|SAMMY WAWERU