Michezo

Jacob Ojee ndiye nahodha mpya wa Shujaa

January 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

JACOB Ojee ameteuliwa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa.

Timu hii itaondoka nchini Jumamosi kushiriki duru mbili zijazo za Raga ya Dunia katika miji ya Hamilton nchini New Zealand (Januari 26-27) na Sydney nchini Australia (Februari 2-3).

Ojee kutoka klabu ya KCB aliwahi kuchezea Shujaa chini ya raia wa Afrika Kusini Paul Treu msimu 2014-2015 akiifungia mguso wa kufuta machozi ikipoteza 38-7 dhidi ya Afrika Kusini katika duru ya Port Elizabeth.

Atasaidiwa majukumu ya unahodha na Michael Wanjala. “Ni heshima kubwa kuteuliwa nahodha wa Shujaa. Si kazi rahisi, lakini na kikosi hiki, naamini tutaimarisha matokeo yetu,” Ojee alisema Januari 16, 2019.

Kocha Mkuu Paul Murunga alimsifu Ojee akisema anao uwezo wa kuongoza Shujaa.

“Tumeona sifa zake za uongozi katika mazoezi anapohakikisha wachezaji wote wanawasiliana. Pia ana uzoefu mkubwa kutoka timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande pamoja na raga ya wachezaji saba kila upande, ambao utakuwa muhimu katika kampeni yetu.  Wanjala pia ana ujuzi aliopata awali katika Raga ya Dunia ambao utatusaidia sana tunapoelekea New Zealand,” Murunga alisema.

Murunga amejumuisha wachezaji watano wapya katika kikosi chake ambao ni Harold Anduvate, Brian Wandera, Eliakim Kichoi na mzawa wa nchi ya Wales, William Reeve.

Wachezaji wengine ni Cyprian Kuto, Johnstone Olindi, Brian Wahinya, Vincent Onyala na Daniel Taabu, ambao walishiriki duru mbili za ufunguzi katika miji ya Dubai (Milki za Kiarabu) na Cape Town (Afrika Kusini) mwezi Desemba mwaka 2018. Bush Mwale anarejea kikosini baada ya kukosa msimu 2017-2018.

Mark Wandetto atasafiri nchini New Zealand na Australia kama mchezaji wa 13. Charles Omondi na Alvin Otieno wako mkekani.

Kenya inashikilia nafasi ya 14 katika ligi hii ya mataifa 15 kwa alama nne. Katika duru ya Hamilton, italimana na mabingwa wa Raga ya Dunia msimu 2017-2018 Afrika Kusini pamoja na Scotland na Ufaransa katika mechi za Kundi C. Afrika Kusini itatangaza kikosi chake Alhamisi alasiri.

Scotland na Ufaransa bado hazijafichua mipango yao ya kutangaza vikosi, lakini zinatarajiwa kufanya hivyo wakati wowote kutoka Alhamisi.

Kikosi cha Shujaa kitakachoshiriki duru za Hamilton Sevens na Sydney Sevens 2019:

Wachezaji – Jacob Ojee (Nahodha, KCB) Michael Wanjala (Nahodha msaidizi, Homeboyz), Cyprian Kuto (Homeboyz), Vincent Onyala (KCB), Brian Wahinya (Blak Blad), Brian Wandera (Homeboyz), Daniel Taabu (Mwamba), Johnstone Olindi (Homeboyz), Bush Mwale (Homeboyz), William Reeve (Kenya Harlequin), Eliakim Kichoi (Mwamba), Harold Anduvate (Menengai Oilers) na Mark Wandetto (Homeboyz). Kocha Mkuu – Paul Murunga.