Kindiki alivyomkaribisha Ruto sherehe za Mashujaa Kwale
NAIBU Rais mteule, Kithure Kindiki ndiye alimlaki Rais William Ruto katika Kaunti ya Kwale kuongoza maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa, inayofanyika leo, Jumapili, Oktoba 20, 2024.
Maadhimisho hayo, yanafanyika Kwale Stadium, siku maalum iliyotengewa kutambua Wakenya wenye michango mbalimbali kwa taifa, wakiwemo waliopigania uhuru wa nchi.
Licha ya kesi zinazomzuia kuapishwa rasmi kuwa mrithi wa Bw Rigathi Gachagua, Prof Kindiki alionekana ‘kutwaa’ majukumu ya unaibu rais, ambaye aghalabu ndiye humwalika rais katika hafla za kitaifa.
Akiwa amevalia suti, Prof Kindiki ambaye Kikatiba angali Waziri wa Usalama wa Ndani, alimlaki Dkt Ruto Kwale kuongoza taifa kuadhimisha Mashujaa Dei 2024.
Rais alitua kwa ndege ya kijeshi, helikopta, akiandamana na mkewe, Mama wa Taifa, Bi Rachael Ruto, pamoja na walinzi wake wa karibu.
“Hujambo, uko salama?” Rais Ruto alimsalimu Prof Kindiki, ambaye alimlaki.
Kiongozi wa nchi, alivalia suti ya Kaunda ambayo imekuwa utambulisho wake.
Bi Ruto, naye alikuwa amevalia kitenge maridadi cha rangi nyekundu na madoadoa meusi.
Naibu Rais mteule alikuwa ameandamana na Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, Waziri wa Biashara, Bw Salim Mvurya, na Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Raymon Omollo.
Rais Ruto alichangamkia kikosi hicho, ambapo baadaye walielekea Kwale Stadium kwa maadhimisho ya Mashujaa Dei 2024.
Prof Kindiki aliteuliwa wiki iliyopita kuwa naibu wa rais, baada ya mtangulizi wake, Rigathi Gachagua kubanduliwa na Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kutia muhuri maamuzi ya wabunge.
Bw Gachagua, aling’atuliwa mamlakani kupitia mswada uliowasilishwa na mbunge wa Kibwezi, Mwengi Mutuse ambapo Seneti ilimvua mamlaka kwa mashtaka matano kwa jumla ya kumi na moja aliyotuhumiwa.
Yanajumuisha ufisadi, kueneza siasa za kikabila na chuki, matumizi mabaya ya ofisi na mamlaka, kati ya mengine.
Bw Gachagua, hata hivyo, kupitia mawakili wake alipata amri ya kusimamisha Prof Kindiki kuapishwa kupitia Mahakama Kuu Nairobi na Kirinyaga (MCA aliwasilisha kesi).
Naibu rais huyo anayeondoka ameapa kupambana na maamuzi ya Seneti kortini, akisema ana imani na idara ya mahakama.