Habari za Kitaifa

Wafanyakazi wa Gachagua wafungiwa nje jumba la Harambee Annex, wakuta kufuli mpya

Na WAANDISHI WETU October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYAKAZI wakuu na wa ngazi za chini wanaofanya kazi katika afisi ya Naibu Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua, walirudishwa nyumbani Jumanne asubuhi waliporipoti kazini katika Harambee House Annex, Nairobi.

Waliozungumza na Taifa Leo walisema walifika na kukuta maafisa mbalimbali wa usalama wakisimamia jengo hilo. Maafisa hao walitoka Kitengo cha Kukabiliana na dharura (RDU).

Maafisa hao hawakuruhusu mtu yeyote kuchukua video au picha. Waandishi wa habari pia hawakuruhusiwa kufanya mahojiano.

“Walituambia tuende nyumbani hadi tutakapofahamishwa,” alisema mmoja wa wakurugenzi wakuu wanaofanya kazi katika afisi ya Bw Gachagua.

Wale wachache waliobahatika kuingia ndani saa za asubuhi walipata kufuli mpya kwenye milango ya ofisi zao na wakalazimika kuondoka.

Haya yalijiri siku chache tu baada ya wafanyakazi 108 wa naibu rais aliyeondolewa madarakani kutumwa kwa likizo ya lazima.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Usimamizi Patrick Mwangi na kunakiliwa kwa Mkuu wa Wafanyakazi na Utumishi wa Umma Felix Koskei, maafisa wote wa daraja la T na U walitumwa kwa likizo.

Taifa Leo iliwasiliana na Bi Njeri Rugene, mkuu wa mawasiliano wa Bw Gachagua, lakini hakujibu simu wala jumbe zetu.

Bw Gachagua amemlaumu Rais William Ruto kwa masaibu yake.

Jana Rais Ruto aliomba Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi kadhaa za kupinga kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais, akidai kuwa masuala yaliyoibuliwa katika kesi hizo yametengewa Mahakama ya Juu pekee.

Dkt Ruto alisema katika majibu yake kwamba kesi zilizowasilishwa zinakiuka Kifungu 140 kama kinavyosomwa pamoja na vifungu vya 148 na 149 vya katiba, ambavyo vinatwika Mahakama ya Juu, mamlaka ya kuamua mizozo inayotokana na mchakato wa uchaguzi wa urais.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 165 (5) (a) cha Katiba, Mahakama hii haiwezi kuamua kesi na kutoa maagizo iliyoombwa, kwa kuwa ni suala ambalo limetengewa Mahakama ya Juu,” Dkt Ruto alisema kupitia wakili Adrian Kamotho.

Bw Gachagua na walalamishi wengine kadhaa walipinga mchakato wa kuondolewa kwake madarakani, kutokana na kutoshirikishwa ipasavyo kwa umma na kushindwa kuthibitishwa kwa madai dhidi yake.

Jaji Chacha Mwita na Richard Mwongo, wa Mahakama Kuu ya Milimani na Mahakama Kuu ya Kerugoya, mtawalia waliidhinisha kesi hizo kuwa za dharura na kusimamisha mchakato wa kujaza nafasi ya Bw Gachagua kama Naibu Rais.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA