Mtakuja kuipenda Adani, asema Rais Ruto akitetea mkataba wa mabilioni
RAIS William Ruto ametetea hadharani mkataba wa Sh95 bilioni unaozingirwa na utata kati ya Kampuni ya Kusambaza Umeme Nchini (Ketraco) na kampuni ya Adani Energy Solutions, akisema mpango huo utapunguza bei za umeme nchini.
Kampuni hiyo pia inahusishwa na mpango wa kukodi uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kwa miaka 30 na mfumo wa tekinolojia wa Afya kwa Wote unaoongozwa na kampuni ya Safaricom.
Mipango inayohusishwa na Adani imepingwa na wadau tofauti waliowasilisha kesi kortini huku serikali ikiitetea vikali. Alhamisi, Rais Ruto alionekana kupuuza wanaopinga mipango inayohusu kampuni hiyo akisifu kandarasi yake na Ketraco.
“Serikali yangu imejitolea kuingia kwenye mikataba na sekta ya kibinafsi kuhusu miradi ya miundomsingi ili kupunguza mzigo wa ushuru na kutegemea deni. Mfano ni mkataba kati ya serikali na Adani Energy Solutions utakaowezesha kupunguza bei ya stima,” alisema.
“Mkataba huu utaepusha kikamilifu hali ya stima kupotea kila mara nchini kupitia nyaya na vituo vipya vitakavyowekwa.”
Mkataba kati ya Ketraco na Adani Energy Solutions Limited, unaokadiriwa kuwa Sh95.68 bilioni, utawezesha kampuni hiyo ya India kubuni, kufadhili, kuunda na kuendesha laini muhimu na vituo vya kusambazia stima kote nchini.
Mkataba huo, kulingana na serikali, unalenga kusuluhisha kero la umeme kupotea kila mara nchini na kuhakikisha kuwepo kwa stima inayoweza kutegemewa kukidhi mahitaji ya uchumi unaozidi kukua nchini na maazimio ya viwanda.
“Wakenya wote wanafahamu changamoto kuu inayokabili taifa letu kutokana na hali ya stima kupotea kila mara. Miradi hii inakusudiwa kuimarisha miundomsingi yetu ya kusambazia umeme kitaifa (nyaya na vituo vya kusambazia umeme), kuhakikisha kuwepo stima inayoweza kukidhi mahitaji ya uchumi wetu,” alisema Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi, aliyezungumza katika hafla hiyo.
Aidha, waziri alisema mradi huo utafadhiliwa na sekta ya kibinafsi huku Adani Energy Solutions ikishughulikia deni.
Katika mkataba huo, Adani itasimamia miundomsingi husika kwa miaka 30 ili kuhakikisha ustawishaji wake kabla ya kuikabidhi Ketraco.
Akitia saini mkataba huo, Oktoba 11, Wandayi alifichua kuwa, Ketraco ilifanya udadisi wa kutosha kuhusu Adani kama mshiriki mkuu wa mradi huo na kushirikisha wadau husika kikamilifu.
Mradi huo unajumuisha ujenzi wa nyaya na vituo vya kusambazia umeme wenye nguvu nyingi ikiwemo mkondo wa Gilgil-Thika-Malaa-Konza wenye 400kV na urefu wa kilomita 208.73.
Utajumuisha ujenzi wa vituo vipya katika miji ya Gilgil, Thika, Malaa, na Konza.
Mkondo wa Rongai-Keringet-Chemosit wenye 220kV line, na urefu wa kilomita 99.98 utajumuisha vituo katika maeneo ya Rongai, Keringet, na Chemosit. Mkondo wa Menengai-Ol Kalou-Rumuruti wenye 132kV na urefu wa kilomita 89.88 na vituo vilivyopo Menengai, Ol Kalou, na Rumuruti na mkondo wa Lessos, 400/220kV.