Habari za Kitaifa

Pesa ziko wapi: Wahadhiri kurejelea mgomo wakishutumu serikali kwa kuwahadaa kuhusu malipo

Na  DAVID MUCHUNGUH October 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAHADHIRI wa vyuo vyote vya umma wataanza mgomo wao leo (Jumanne) baada ya Muungano wa Wahadhari na Wafanyakazi wa Vyuo (UASU) na serikali kukosa kuelewana kuhusu utekelezaji wa mkataba wa kurudi kazini uliotiwa sahihi Septemba 26 mwaka huu.

Mgomo huu unatarajiwa kuvuruga shughuli za masomo vyuoni.

Katibu Mkuu wa UASU Constantine Wasonga aliwaelekeza wanachama wasifanye kazi hadi serikali iwaongezee mishahara kwa mujibu wa makubaliano.

Dkt Wasonga alituhumu serikali kwa kuwahadaa na akasema hawawezi kuingia kazini hadi wapokee mishahara kwenye akaunti za benki.

“Fanyeni kazi leo (Jumatatu) hadi usiku saa sita. Baada ya dakika moja, bwageni zana za kazi. Kusiwe na ufunzaji darasani ama kwa njia ya kidijitali, kusahihisha ama kusimamia mitihani hadi mpokee pesa zenu,” alisema Jumatatu baada ya kusimamia mkutano wa Baraza la Kitaifa la UASU jijini Nairobi.

Katika mkataba wa kurudi kazini, wahadhiri wa viwango vya chini wanatarajiwa kupata nyongeza ya asilimia 10 huku walio katika viwango vya juu wakipata nyongeza ya asilimia saba kwa mishahara yao pamoja na nyongeza ya moja kwa moja ya asilimia 4 kwa mshahara wa msingi kila mwaka.

Nyongeza hii inafaa kuonekana katika mishahara ya miaka miwili kati ya (2023-2024 na 2024-2025) na kutekelezwa kwenye mishahara ya Oktoba 2024.

Makubaliano ya kurejea kazini baada ya mgomo yalipigwa jeki na Waziri wa Leba Alfred Mutua.

Mgomo huo ulihusisha wafanyakazi wengine wa vyuo waliowakilishwa na Muungano wa wafanyakazi wa Vyuo (KUSU) na ule wa wafanyakazi wa hoteli na hospitali (KUDHEIHA).

Lakini vyama hivi havijatoa taarifa kuhusu mkataba wao na serikali na hawakuwa pamoja na viongozi wa UASU walipotoa taarifa kwa vyombo vya habari.

“Siwezi kuzungumza kuhusu miungano mingine. Iwapo wamekubali, ni vizuri kwao. Mimi ninawakilisha wanachama wa UASU,” alisema Dkt Wasonga alipoulizwa kama vyama hivyo vitashiriki mgomo.