Kinda mtahiniwa wa KCSE anayeugua selimundu aomba wahisani wamchangie apate matibabu
HUKU Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) ukikaribia kuanza wiki ijayo, Ned Gori ambaye ni mtahiniwa amelazwa katika hospitali ya Kenyatta.
Kama wanafunzi wenzake katika Shule ya Upili ya Dagoretti, Ned anapaswa kudurusu akisubiri mtihani ila hawezi kwani anapambana na maumivu.
Mamake, Bi Florence Atieno, ameketi kando ya kitanda chake akimuuguza. Mnamo Jumatatu Novemba 4, 2024, atakuwa miongoni mwa watakaoanza mitihani yao ya KCSE.
Tangu Ned alipopatikana na ugonjwa wa selimundu alipokuwa na umri wa miezi minne tu, maisha yake yamekuwa ya taabu kwani yeye mara nyingi huwa hospitalini akipokea matibabu.
“Anataka kuwa kama wengine, lakini ugonjwa haumruhusu,” mama yake alisema huku sauti yake ikijaa machungu.
Kwa miaka 18 iliyopita, Bi Florence amekuwa karibu na mwanawe, kwa kukosa usingizi usiku na kulazwa hospitalini bila kikomo na maumivu.
“Daktari alisema itagharimu Sh12 milioni kumpeleka India kwa matibabu. Nimejaribu kila kitu lakini bado tuko mbali sana na kupata kiasi hicho cha pesa. Naomba msaada kwani sitaki kumpoteza mwanangu. Yeye ni kila kitu kwangu, nuru yangu, na wazo la yeye kufa kwa sababu sikuweza kupata njia ya kumwokoa inaniuma sana. Tafadhali, ninahitaji msaada,” akasema Bi Florence.
Wasamaria wema wanaweza kumsaidia Ned kupitia PAYBILL NUMBER: 4230034, AKAUNTI JINA: NED GORI MEDICAL FUND, NAMBA YA AKAUNTI: NED MEDICAL.