Jamvi La Siasa

Sitakuangusha, Kindiki aambia Ruto akianza kazi

Na JUSTUS OCHIENG November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Prof Kithure Kindiki ameahidi Rais William Ruto kwamba, ataheshimu kiapo cha afisi yake kwa kuwa mwaminifu na kutumikia nchi bila woga wala upendeleo wowote.

Katika hotuba baada ya kuapishwa kwake kuwa naibu rais wa tatu wa Kenya iliyoshuhudiwa na kiongozi wa nchi, Prof Kindiki alisema atasalia kuwa mtiifu na kuhudumu kwa uaminifu kama msaidizi rasmi wa rais kikatiba.

‘Kwa kiapo cha utiifu na utekelezaji wa majukumu ya Naibu Rais nilicholishwa, nataka kuahidi mbele ya mkutano huu na Mwenyezi Mungu kwamba, nitahudumu chini yako na kukupa usaidizi unaohitaji ili kuipeleka nchi hii katika ngazi ya juu zaidi, nitakuwa mtiifu na mwaminifu,’ Prof Kindiki alisema.

Naibu Rais pia alisema atafanya bidii kumpunguzia Rais Ruto mzigo mabegani mwake anapojitahidi kuwahudumia Wakenya.

‘Leo hii, hii ni heshima ya juu zaidi katika maisha yangu na siichukulii kuwa ya kawaida,’ akasema Naibu Rais Kindiki.

Aliendelea: ‘Sina maneno kuelezea jinsi ninavyoshukuru leo. Ninamshukuru Mungu, wewe mheshimiwa ( Rais Ruto) kwa heshima uliyonipa kuhudumu chini yako.

‘Nimekuwa mwanafunzi wako kisiasa kwa karibu miaka 20 sasa. Ninaahidi mbele ya mkutano huu na Mungu kwamba sitawaangusha kwa heshima uliyonipa.’

Prof Kindiki alisema anashukuru taasisi zote zilizofanikisha mchakato mzima ikiwemo sherehe ya kumuapisha.

‘Huu ni thibitisho ya ukomavu wa demokrasia yetu na inathibitisha kwamba, taasisi zetu zinafanya kazi. Ninapoondoa mzigo kwenye mabega yako, ninaahidi kwamba nitakutumikia kwa bidii.’

Naibu Rais alipongeza familia yake na mkewe kwa kuandaa msingi wa mafanikio yake.

‘Nawashukuru wote ikiwa ni pamoja na familia yangu, mke wangu Dkt Joyce Kithure na watoto wangu watatu kwa kuwa msingi na kutoa usaidizi ambao nimekuwa nikihitaji kila mara katika nyanja hii.’

Aliendelea: ‘Ninathibitisha katika safari yangu yote inayofikia kilele wakati huu, nimeamini kuwa katika Kenya kila kitu kinawezekana. Kwa mtu kama mimi kuchukua wadhifa wa Naibu Rais, inaweza tu kutokea nchini Kenya.’

Rais William Ruto alisema ana imani kuwa Naibu Rais Kithure Kindiki atampa usaidizi unaohitajika katika kuongoza nchi ambao amekosa kwa miaka miwili iliyopita.

Akionekana kumlenga naibu wake aliyetimuliwa mamlakani Rigathi Gachagua, Dkt Ruto alisema Prof Kindiki yuko tayari kutumikia Jamhuri ya Kenya bila kupendelea eneo lolote.

‘Ninahitaji sauti na akili yako kuhusu mambo tunayofanya (kama serikali) kwani nimekuwa nikikosa hilo kwa miaka miwili iliyopita,’ rais alimweleza Kindiki wakati wa kuapishwa kwake.

‘Tunahudumu kwa heshima ya watu wa Kenya. Hakuna hata mmoja wetu aliye juu kuliko Katiba inavyosema. Ni lazima tutii Katiba.’

Kiongozi wa nchi alisema Wakenya ni jamii moja chini ya taifa moja kuu.

‘Tutahudumia watu wote kwa usawa. Hakuna eneo au jamii itakayosalia nyuma. Tutahudumia waliotupigia kura na wale ambao hawakutupigia kura kwa usawa,’ Ruto alisema.

Rais alimtaja Prof Kindiki kuwa msimamizi mwaminifu wa Ajenda ya Uchumi ya kuanzia mashinani ya serikali ya Kenya Kwanza.

Profesa Kindiki aliapishwa katika hafla ya kufana iliyofanyika nje ya Jumba la la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta (KICC) iliyoshuhudiwa na Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome, miongoni mwa wageni mashuhuri.

Viongozi wengine walioshuhudia hafla hiyo ni pamoja na Mawaziri wakiwemo Hassan Joho, Davis Chirchir, Opiyo Wandayi, Julius Ogamba, Justin Muturi na Aden Duale.

Baadhi ya magavana walikuwepo ni Muthomi Njuki (Tharaka Nithi, Cecily Mbarire (Embu), Susan Kihika, Paul Otuoma (Busia), Stephen Sang (Nandi) na Abdi Guyo (Isiolo).

Imetafsiriwa na Benson Matheka