Kiapo cha Kindiki chafungua ukurasa wa mkewe kujulikana
MKE wa Naibu Rais Daktari Joyce Gatiria Njagi Kithure, aliteka mioyo ya Wakenya wakati wa kuapishwa kwa Naibu Rais Kithure Kindiki, Ijumaa Novemba 1, 2024.
Dkt Joyce Gatiria Njagi Kithure aliwavutia Wakenya alipotembea akiwa wameshikana mikono na Naibu Rais wa tatu wa Kenya, Profesa Kindiki huku wakitembelea kwenye zulia jekundu kuelekea kwenye eneo la kiapo.
Huku mumewe akiendelea kuvuna umaarufu, Dkt Kithure ameepuka kuwepo machoni mwa umma.
Wawili hao walifunga ndoa 2001 na kufanikiwa na watoto watatu,
Mama huyu wa watoto watatu alijitokeza kadamnasi mbele ya Wakenya Novemba 1, 2024 watu wengi wakitaka kumjua ‘Mama wa Taifa wa Pili.’
Dkt Kithure alipata fursa ya alitangamana na watu mashuhuri serikalini na kufungua maisha yake kwa kurunzi ya umma – ni baada ya mumewe kupanda ngazi kisiasa na kihadhi alipoibuka kuwa mtu wa pili mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini.
Heshima
Alipoamkuana na viongozi mbalimbali, Dkt Kithure alidhihirisha heshima na unyenyekevu.
Kila aliponyoosha mkono kwa salama, alionekana akiwa ameushikilia mkono wake wa kulia kwa ishara ya heshima.
Naibu Rais Prof Kindiki alimtaja mkewe akisema kuwa amechangia sana kufanikisha safari yake ya siasa.
Alieleza kuwa Joyce alijinyima kujitolea zaidi kazini mwake ili kuhakikisha mazingira ya familia yao yanakuwa shwari.
Aghalabu Dkt Kindiki alifanya hivi wakati Prof Kindiki amekuwa katika shughuli nyingi za kikazi nchini na kimataifa.
“Nataka kutoa pongezi kwa watu wanne ambao wamejitolea sana, haswa katika kipindi cha miaka 15 hivi nimekuwa kwenye siasa,” alisema Profesa Kindiki.
Bw Kindiki alishukuru wanawe watatu ambao ni Imani, Neema, na Mwende, ambao wamekuwa na Dkt Kithure alipokuwa akitekeleza majukumu ya taifa.
Hajulikani sana
Ni machache mno yanajulikana kumhusu Dkt Kithure licha ya kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Anafahamika kutoka katika familia ya kawaida, na kuwa na bidii kutafuta elimu ambayo imemwezesha kupata shahada ya uzamifu na kuwa mhadhiri wa kiwango cha juu.
Yeye ni msomi mwenye Shahada ya Kwanza ya Sayansi, Shahada ya Uzamili katika Sayansi, na Shahada ya Uzamifu katika Kemia ya Mazingira.
Alifuzu kwa Shahada ya Uzamifu katika Kemia ya Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 2013.
Daktari Kithure ni mcha Mungu kama mtangulizi wake (Bi Dorcas Rigathi).
Hii ni baada ya kujitambulisha kuwa kifungua mimba katika familia yake na kuokoka wakati wa ibada ya mazishi ya babake.
Ni mhadhiri mkuu katika Chuo Kikuu cha Nairobi katika Idara ya Kemia ambako amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10.
Akiwa Mke wa kiongozi wa Pili nchini, Dkt Kithure bila shaka ataendeleza dhamira yake ya kuleta mabadiliko chanya na kuwainua wanaohitaji elimu.