Makala

Magunia ya pesa yalivyotolewa ndani ya nyumba ya Dada Mary

Na FRIDAH OKACHI November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KANISA la Jerusalem Church of Christ lililoasisiwa na ‘Nabii’ Mary Sinaida Akatsa almaarufu Dada Mary, lina wafuasi 6,000 ambao hushiriki ibada katika matawi matano ya dhehebu hilo nchini, manne yakiwa katika Kaunti za Vihiga na Kakamega.

Katika mtaa wa Kawangware 56, Nairobi palipo na makao makuu ya kanisa hilo, mita 20 kutoka kituo cha kuegesha magari, wafuasi wake hukutana kufanya mipango ya mazishi ya Dada Mary, 64 aliyefariki Oktoba 26, 2024.

Mipango hiyo inajumuisha kutafuta mrithi wake kabla ya kuzikwa kwake.

Inadokezwa kuwa kabla ya kuzikwa kwa mwazilishi wa kanisa hilo, Dada Mary, kuna rafiki wa karibu wa nabii huyo ambaye atatakaswa (kutawazwa mrithi wake).

Unapokaribia nyumbani kwake, lango ambalo lilikuwa limechakaa kwa sasa limepakwa rangi huku shughuli mbalimbali zikiendelea, kinyume na hapo awali.

Baada ya Taifa Leo kubaini kuwa Akatsa aliishi katika mtaa wa kichochole, kinyume na wanawe wanaoishi mtaa wa Karen, Nairobi, imefichuka kuwa Mzee wa Nyumba Kumi alishuhudia jinsi magunia yanayoaminika kuwa na pesa yalivyochukuliwa na polisi.

“Maafisa wa polisi na wakili wa familia walikuja kuchukua na kupeleka mabunda hayo ya pesa kwenye benki,” anasema mzee huyo.

Je, Dada Mary alijikimu vipi? Ufadhili, sadaka na ada za usajili.

Aliyekuwa mfuasi wa kanisa hilo lililoanzishwa katika miaka ya 1980, Bi Margret Nasa Wambua anaeleza kuwa baada ya kanisa hilo kuhama kutoka eneo la Muslim, Kawangware hadi Kawangware 56, mwazilishi wake aliwahimiza kulipia pesa za usajili.

Mapema miaka ya 1990, kila mfuasi alijisajili kwa Sh20 pekee.

Usajili huo uliwawezesha kupata kadi na kutambuliwa kama wafuasi.

“Kulingana na kadi ya kanisa nilikuwa nambari 360 baada ya kujisajili kwa Sh20. Waliojiunga nasi walilipia zaidi mbali na sadaka ya kawaida,” alisema Bi Wambua.

Mfuasi mmoja wa sasa alisema kuwa pesa hizo zilitumika kuwasaidia washirika wao ambao pia walipatwa na changamoto kama vile malimbikizi ya kodi ya nyumba katika jiji la Nairobi. Hata hivyo, anaeleza kuwa mwinjilisti huyo alikuwa na wafadhili ambao wamekuwa wakimwezesha kuendeleza shughuli za kanisa hilo.

Inakisiwa kuwa hii ni mojawapo ya njia ambazo zilimwezesha Dada Mary kupata pesa zilizopatikana nyumbani kwake.

“Maisha yanabadilika kila wakati, sasa hivi usajili uliongezeka. Usajili huo umetuwezesha kufanya shughuli zetu bila kutatizika,” alisema mfuasi huyo.

Bi Akatsa pia aliwavutia watu wengine kutoka nje ya Nairobi kuishi Nairobi.

Bi Dorothy Maradi alisema mwaka wa 1993 alifika jijini ili kukutana na mhubiri huyo baada ya kuugua muda mrefu.  Hii ni baada ya mjomba wake kuwasimulia kuhusu sifa za Akatsa.

“Nilipofika na jamaa yangu tulielekezwa kwenye uwanja ambapo alikamilisha maombi yake saa moja jioni. Nilipona na nikahimizwa kuwa nyumbani sio kwema,” alisema Bi Maradi. Uponyaji huo ulimfanya kusalia mtaani humo kwa zaidi ya miaka 30 bila kurejea kwao.

Taifa Leo ilibaini kuwa kuna baadhi ya mabinti wanaoitwa Sinaida kama msalihina huyo.

Sinaida Wambui, 29, anasema kuwa mamake mzazi alimfahamisha kuwa jina hilo linatokana na nabii huyo aliyeamrisha aitwe vile.

“Huwa nafurahi sana kuitwa hivyo, maana wazazi wangu walitatizika kupata mtoto. Nilipozaliwa nikapewa hilo jina,” akaeleza Bi Wambui.