Habari za Kitaifa

Msako waanza Equatorial Guinea kufuatia kuvuja kwa video za ngono za afisa wa ngazi za juu serikalini

Na REUTERS, CHARLES WASONGA November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MALABO, Equitorial Guinea

TAIFA la Equatorial Guinea Jumanne limetoa amri ya kuandamwa kwa maafisa wa serikali wanaoshiriki ngono afisini na waadhibiwe vikali.

Hii ni baada ya kanda za video kusambaa mitandaoni zikionyesha afisa mmoja wa cheo cha juu katika wizara ya fedha akila uroda na wanawake sehemu kadhaa, ikiwemo afisini mwake.

Serikali ilisema imechukua hatua hiyo kwa sababu kanda za video kama hizo zinaharibu sifa na hadhi ya taifa hilo dogo lililoko Afrika Magharibi.

Taharuki imetanda nchini Equatorial Guinea tangu video kama hizo kuvuja mitandaoni wiki jana.

Kulingana na taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari, mamia ya video, zisizo za kitaalamu, zimepatikana katika makazi ya afisa huyo wa wizara ya fedha wakati wa msako kuhusu sakata moja ya ufisadi.

Wanawake walioonekana katika kanda hizo za video wanaonekana kujumuisha wake za maafisa wenye vyeo vya juu katika serikali ya Equatorial Guinea na watu wa familia zao, kulingana na vyombo vya habari nchini humo.

Shirika la habari la Reuters halikufaulu kuthibitisha uhalisia wa video hizo.

Mnamo Jumanne, Novemba 5, 2024 Makamu wa Rais Nguema Obiang Mangue aliamuru kufanyika kwa msako wa maafisa wa serikali wanaoshiriki ngono afisini ili kuzima kabisa visa hivyo.

“Serikali inalenga kuzuia visa hivyo vya aina ambapo maafisa wa wizara mbalimbali za serikali na hata idara ya mahakama hushiriki ngono haramu wakiwa kazini,” ikaeleza taarifa kutoka afisi ya Makamu ya Rais.

Mikakati ambayo serikali imechukua kuzuia vitendo hivyo vya aibu ni pamoja na kuweka kamera za usalama katika afisi zote za umma na kuanzisha doria za maafisa wa usalama katika afisi hizo; mchana na usiku.

Taarifa hiyo ilisema hatua hizo zilifikiwa wakati wa mikutano ya dharura wakuu wa Mahakama ya Kuu, Afisi ya Mwanasheria Mkuu na maafisa wakuu katika wizara zote za serikali.

Iliamuliwa kuwa wale ambao walionekana kwenye kanda za video za ngono watasimamishwa kazi kwa muda, japo majina yao hayakutolewa.

Aidha, iliamuliwa kuwa wale waliotwikwa jukumu la kulinda majengo ambamo video hizo zilinakiliwa wataadhibiwa kwa kufeli kutekeleza majukumu yao.

Taifa la Equatorial Guinea, lenye jumla ya watu milioni 1.7 pekee, limeongozwa na Rais Teodoro Obiang kwa kipindi cha miaka 45.

Kiongozi huyo ndiye anashikilia rekodi ya dunia kama rais aliyehudumu kwa miaka mingi zaidi.