Jamvi La Siasa

Chama cha Trump chabwaga Democratic cha Harris na kutwaa udhibiti wa Seneti

Na BENSON MATHEKA, MASHIRIKA November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha Republican kilishinda viti vingi katika Seneti ya Amerika na kunyakua udhibiti kutoka kwa Democratic, vyombo vya habari vya Amerika vilikadiria mapema Jumatano.

Ushindi huo unamaanisha kuwa rais ajaye akitoka chama hicho atapata uungwaji mkono mkubwa wa kutunga ajenda zake na kuteua majaji katika Mahakama ya Juu ya Amerika.

Donald Trump wa The Republican anaongoza katika kura urais dhidi ya Kamala Harris wa chama cha Democratic.

Bunge la Amerika limegawanywa katika Bunge la Wawakilishi — ambapo viti vyote 435 vinawaniwa — na Seneti yenye wajumbe 100, ambayo ina viti 34 vilivyokuwa vikipiganiwa mwaka huu. Uchaguzi wa Congress unaendeshwa pamoja na wa urais.

Jim Justice, gavana  wa Republican jimbo la Virginia Magharibi, aliwafurahisha Wanarepublican mapema usiku alipoibuka mshindi kwa urahisi katika kinyang’anyiro cha Seneti kuchukua nafasi ya Joe Manchin aliyekuwa akistaafu.

Ohio kisha ikaingia kwenye safu ya Republican baada ya Seneta wa muda mrefu wa Democratic, Sherrod Brown kushindwa na Bernie Moreno, mfanyabiashara aliyeidhinishwa na Trump na mtoto wa afisa wa wakati mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Colombia.

Fox News na ABC zilitangaza ushindi wa Republican katika seneti baada ya Seneta wa Republican Deb Fischer kujikinga na changamoto kubwa isiyotarajiwa kutoka kwa mwaniaji huru huko Nebraska.

“Ninatazamia kufanya kazi na Rais Trump na wengi wetu wapya wa kihafidhina ili kuifanya Amerika kuwa kubwa tena kwa kuifanya Seneti kufanya kazi tena,” Seneta wa Texas John Cornyn wa Republican, alisema katika taarifa.

Ushindi wa Justice na Moreno ulibatilisha uthibiti wa Seneti wa Democrats wa 51-49, huku Wanarepublican wakitazamia kuendeleza uongozi wao zaidi na uwezekano wa kushinda Montana, Wisconsin na Pennsylvania.