Trump ajitangaza mshindi wa urais, ashukuru wafuasi wake kwa kufanya makubwa
DONALD Trump wa chama cha Republican, Jumatano ameshinda kinyang’anyiro cha urais baada ya Fox News kukadiria kwamba alikuwa amemshinda Kamala Harris wa Democratic, jambo ambalo limerejesha ushawishi wake kisiasa miaka minne baada ya kuondoka Ikulu ya White House.
“Amerika imetupa mamlaka ambayo haijawahi kufanyaka na yenye nguvu,” alisema mapema Jumatano akihutubia umati wa wafuasi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kaunti, Palm Beach.
Vyombo vingine vya habari havikuwa vimetangaza mshindi wa kinyang’anyiro cha urais, lakini alionekana kukaribia kushinda baada ya kuwa kifua mbele katika majimbo yenye ushindani ya Pennsylvania, North Carolina na Georgia na kuongoza katika mengine manne, kulingana na Edison Research.
Harris hakuzungumza na wafuasi wake, ambao walikuwa wamekusanyika katika chuo kikuu cha Howard. Mwenyekiti mwenza wa kampeni ya Harris Cedric Richmond, alihutubia umati kwa kifupi baada ya saa sita usiku, akisema Harris atazungumza hadharani siku ya Jumatano.
“Bado tuna kura zinazoendelea kuhesabiwa,” alisema.
Rais huyo wa zamani alikuwa akiongoza katika maeneo mengi ya nchi, akiboresha utendaji wake alioandikisha 2020 kila mahali kuanzia maeneo ya mashambani hadi mijini.
Wanarepublican walishinda viti vingi katika seneti vilivyoshikiliwa na Democratic katika majimbo ya West Virginia na Ohio.
Hakuna chama chochote kilichoonekana kuwa na makali katika vita vya kuwania udhibiti wa Bunge la Wawakilishi ambapo Wanarepublican kwa sasa wanashikilia uongozi lakini mwembamba sana.
“Tunaongoza seneti na inaonekana tutafanya hivyo katika Bunge la Wawakilishi,” Trump aliambia wafuasi wake akiwalimbikizia sifa tele kwa kusimama naye wakati wa kampeni na wakati wa kura.
Trump alipata uungwaji mkono zaidi kutoka kwa Wahispania, wapiga kura wa jadi wa chama cha Democratic, na familia za kipato cha chini ambazo zimehisi kufinywa na kupanda kwa bei tangu uchaguzi uliopita wa rais wa 2020, kulingana na kura za maoni kutoka shirika la Edison.
Trump alishinda asilimia 45 ya wapiga kura wa Uhispania kote nchini, akimfuata Harris kwa asilimia 53.
Takriban asilimia 31 ya wapiga kura walisema uchumi ndio suala lao kuu, na walimpigia kura Trump kwa asilimia 79, kulingana na kura za maoni. Asilimia 45 ya wapiga kura kote nchini walisema hali ya kifedha ya familia zao ilikuwa mbaya zaidi leo kuliko miaka minne iliyopita, na walimpendelea Trump.