Afya na Jamii

Jiandaeni sasa kula GMO baada ya mahakama kusema imeridhika na jinsi athari zitashughulikiwa

November 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imezima kesi kadhaa zinazopinga hatua ya serikali ya kuondoa marufuku dhidi ya matumizi ya vyakula vilivyozalishwa kisayansi (GMO), ikisema suala hilo lilikuwa limeshughulikiwa na Mahakama ya Mazingira na Ardhi mwaka jana.

Kwenye taarifa ya Oktoba 2022, baraza la mawaziri liliondoa marufuku hiyo iliyowekwa miaka 10 iliyopita.

Hatua hiyo ilichangia kesi kadhaa kuwasilishwa kortini kwa hofu kwamba vyakula vya GMO vina madhara kwa afya ya binadamu, wanyama, mazingira na mimea asili.

Miongoni mwa waliowasilisha kesi kortini ni wakili Paul Mwangi aliyelalamika kuwa kuondelewa kwa marufuku dhidi ya vyakula wa GMO kulifanywa haraka na bila ushirikishaji wa maoni ya umma.

Aidha, wakili huyo alisema kuwa hatua hiyo inakiuka haki za wakulima wenye mashamba madogo na watumiaji bidhaa za mashambani.

Bw Mwangi alisema kuwa kuondolewa kwa marufuku hiyo kutachangia kudidimia kwa mbegu za kiasili na kutoa nafasi kwa kukita kwa biashara ya kulinda mbegu za GMO.

Hata hivyo, Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi alisema kwamba mahakama inayosikiliza kesi za mazingira na ardhi ilishughulikia kesi kama hiyo mwaka jana na kuamua kwamba serikali imeweka mikakati ya kushughulikia hofu iliyoibuliwa na walalamishi.

Kwenye uamuzi alioutoa Oktoba mwaka jana, Jaji Oscar Angote alisema serikali imeweka masharti ya kisheria ambayo sharti yatimizwe kabla ya uagizaji au ukuzaji wa vyakula vya GMO.

“Kwa msingi huu, mahakama hii inaamua kuwa kesi hii haina msingi wowote. Kesi hiyo imeondolewa bila agizo kutolewa kuhusu gharama,” Jaji Mugambi akasema. Bw Mwangi alisema hofu kubwa ni uwezekano wa kuingizwa nchini kwa vyakula vilivyozalishwa kupitia teknolojia ya kuzima kabisa uwezekano wa mmea huo kuzalisha mbegu zinazoweza kupandwa kwingineko.

Teknolojia hiyo inajulikana kwa Kimombo kama Genetic Use Restriction Technology (GURT). Vyakula vya GMO vilipigwa marufuku nchini na utawala wa rais wa zamani Mwai Kibaki mnamo 2012.

Marufuku hiyo ilidumishwa kwa miaka 10 chini ya utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Lakini utawala wa Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto uliondoa marufuku hiyo Oktoba 3, 2022 na hatua hiyo ikachapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali mnamo Oktoba 26, 2022.

Serikali ya Rais Ruto ilisema ilichukua hatua hiyo kama mojawapo ya hatua za kupunguza bei ya chakula nchini.Watafiti nchini wamekuwa wakiifanyia majaribio aina ya mahindi ya GMO ambayo inaweza kustahimili kiangazi na wadudu waharibifu.

Katika uamuzi wake, Jaji Mugambi alisema Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilishughulikia suala la kuondolewa kwa marufuku hiyo na masharti ya usalama yaliyowekwa na kubaini kuwa sheria zilizopo zinaendana na haja ya udumishaji wa usafi na ubora wa mazingira.

Jaji huyo aliongeza kuwa mahakama ya mazingira inayo mamlaka sawa na Mahakama Kuu na kwa kuwa imeshughulikia suala hilo, Mahakama Kuu haiwezi kulishughulikia tena.

Katika uamuzi wa mwaka jana, Jaji Angote alisema kulingana na Sheria kuhusu Usalama wa Viumbe Asili, Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Usalama wa Viumbe Asili (NBA) kwa ushirikiano na idara ya afya ya umma imeweka sheria thabiti ya kulinda umma dhidi ya vyakula vibaya.

Imetafsiriwa na CHARLES WASONGA